Tanzania yatahadharisha mlipuko homa ya uti wa mgongo

September 17, 2021 6:33 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ugonjwa huo umelipotiwa katika jimbo la Tshopo, Congo DRC.
  • Huambukizwa kwa njia ya hewa au kukaa na mtu mwenye maambukizi.
  • Serikali yasema inafuatilia kwa karibu ugonjwa huo, wananchi watakiwa kuchukua tahadhari.

Dar es Salaam. Serikali  ya Tanzania imesema inafuatilia kwa karibu mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC Congo) huku ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kuepuka mikusanyiko ya watu wengi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa Septemba 8, 2021 na Shirika la Afya Duniani (WHO) ugonjwa huo umelipotiwa katika jimbo la Tshopo ambapo watu 261 wameripotiwa kuugua na 129 kufariki dunia. 

Ugonjwa huo unaoambukiza husababishwa na bakteria wanaojulikana kama ‘Neisseria meningitidis’ ni tishio kwa sasa barani Afrika.

Vimelea vya ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa au kukaa na mtu mwenye maambukizi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale amesema ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari kwani magonjwa hayana mipaka, hususani mikoa inayopakana na Congo DRC.

Dk Sichwale amesema Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo nchini DRC na kuchukua hatua ili kuzuia na kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo endapo utajitokeza nchini.

Ameelekeza mikoa yote inayopakana na Congo DRC ikiwemo Kigoma, Rukwa, Kagera, Katavi na Songwe kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huo na utoaji taarifa kupitia mfumo wa utoaji taarifa za magonjwa ya mlipuko.

“Naagiza kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa katika ngazi ya jamii hususani maeneo ya mipakani ili kutambua mapema mgonjwa na kuwaandaa watoa huduma na vituo vya huduma kukabiliana na ugonjwa huu endapo utajitokeza,” amesema Dk Sichwale katika taarifa yake iliyotolewa Septemba 16, 2021.

Mikoa hiyo ya mipakani imetakiwa kuongeza nguvu ya ufuatiliaji katika mipaka, hususani kwa wageni wanaoingia nchini kutoka DRC.

Ugonjwa huo hushambulia uti wa mgongo na unaweza kusababisha ulemavu na kifo. Picha| HealthCare AtHome.

Dalili na wajibu wa wananchi

Kwa  mujibu wa Wizara ya Afya, ugonjwa ugonjwa huo huchukua siku mbili hadi 10 tangu kuambukizwa hadi mtu kuanza kuonyesha dalili.

Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa kali, kichwa kuuma, kutapika, kuogopa mwanga, kuchanganyikiwa na shingo kukakamaa.

Dk Sichwale amesema ugonjwa huo unaweza sababisha madhara makubwa kwenye ubongo, kupotea kwa usikivu au ulemavu mwingine wa kudumu na hata kupoteza maisha, hivyo tahadhari inapaswa kuchukuliwa.

Ili kuzuia maambukizi wananchi wameelekezwa kuepuka mikusanyiko ya watu wengi hasa wakati wa milipuko, makazi yazingatie mzunguko mzuri wa hewa. 

“Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa mapema endapo wataona mtu yeyote mwenye dalili zilizotajwa ili hatua stahiki za kudhibiti zichukuliwe mapema,” amesema.

Amewasisitiza wananchi wasiwe na wasiwasi bali waendelee kuzingatia kanuni za afya muda wote.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW