Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Mpox (Monkeypox)

August 19, 2024 12:16 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuepuka kugusana na mtu mwenye dalili za Mpox. 

Kutokana na kuongezeka kwa visa vya wagonjwa wa Mpox katika nchi jirani kama Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Wizara ya Afya ya Tanzania imetoa tahadhari na njia za kuchukua ili kujikinga na ugonjwa huo.

Wizara ya Afya inatoa angalizo hilo ikiwa ni wiki moja tangu Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) wautangaze ugonjwa huo kuwa janga la dharura barani Afrika na maeneo mengine duniani.

Kwa mujibu wa CDC hadi kufikia mwaka 2024, nchi zilizoathirika zimethibitisha jumla ya kesi 2,863 na vifo 517, hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 

Kesi zinazoshukiwa barani Afrika zimeongezeka kwa kasi, zikifikia zaidi ya 17,000, ongezeko kubwa kutoka kesi 7,146 mwaka 2022 na kesi 14,957 mwaka 2023.

Kutokana na kuongezeka kwa visa hivyo katika maeneo mengine barani Afrika hususan katika nchi jirani za Kenya na DRC, Wizara ya Afya imeanisha njia za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuepuka kugusa maji maji ya mgonjwa.

“Epuka kusalimiana kwa kukumbatiana, kubusiana au kushikana mikono na mtu mwenye maambukizi ya Mpox,” imesema taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa hivi karibuni kupitia ukurasa wa Instagram.

Njia nyingine zilizoainishwa na wizara hiyo ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kula, kugusa mizoga au wanyama pori, kusogeleana karibu na mtu mwenye dalili za Mpox, kuepuka kugusa vifaa, nguo, au godoro la mtu mwenye maambukizi ya Mpox na kuvaa barakoa iwapo unamkaribia mtu wenye dalili za Mpox.

Pia wizara hiyo imeshauri kuziba mdomo kwa kitambaa safi wakati wote unapokohoa au kupiga chafya, kusafisha na kutakasa sehemu zote na vitu ambavyo vinaguswa mara kwa mara.

Virusi vya mpox vinavyoonekana katika picha / Picha Vatican News

Ufahamu ugonjwa wa  Mpox (Monkeypox)

Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) Mpox (monkeypox) ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya monkeypox (MPXV) ambavyo ni virusi vya jini ya Orthopoxvirus. 

Ugonjwa huu huathiri binadamu na wanyama kama vile nyani, panya, paka, mbwa.

Dalili za Mpox zinaweza kujitokeza kati ya siku moja hadi 21 baada ya kuambukizwa na mara nyingi hudumu kwa wiki mbili hadi nne.

Dalili hizo ni pamoja na upele unaojitokeza na baadae kuwa vidonda, homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, uchovu na kuvimba kwa tezi za mwili.

Mpox huambukizwa kwa kugusa vidonda vya ngozi vya mtu aliyeambukizwa, kubusiana, kufanya ngono, kushika nguo au mate ya mtu mwenye maambukizi.

Enable Notifications OK No thanks