Si kweli: Baking soda, chai ya manjano inatibu Mpox
- Wizara ya afya yasema hakuna tiba kamili ya ugonjwa huo, ila mgonjwa atatibiwa kwa mujibu wa dalili anazoonyesha,.
- WHO yasema viungo hivyo vya jikoni haviwezi kutumika kutibu ugonjwa huo.
Arusha. Siku chache baada ya Tanzania kuthibisha uwepo wa ugonjwa wa Mpox baadhi ya watu wamekuwa wakihamasisha matumizi ya baadhi ya viungo vya jikoni kama baking soda na manjano kutibu ugonjwa huo kupitia mitandao ya kijamii jambo ambalo si kweli.
Machi 10, 2025 Wizara ya Afya ilibaini watu wawili kuwa na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox ikiwa ni mara ya kwanza kwa ugonjwa huo kuingia nchini Tanzania.
Tangu kuripotiwa kwa ugonjwa huo kumekuwa na taarifa nyingi zinazowaelekeza wananchi jinsi ya kujikinga na kujitibu na ugonjwa huo kinyume na mwongozo wa Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Taarifa hizo zinasambazwa kupitia mitandao mbalimbali ikiwemo Instagram zinadai matumizi ya viungo vya jikoni ikiwemo baking soda vinaweza kumpa nafuu mgonjwa wa mpox endapo atajipakaa mwilini au kuogea huku wengine wakishauri unywaji wa chai ya manjano iliyochanganywa na viungo vingine kama tangawizi kutibu ugonjwa huo.
“Hii kitu ikikupata jitahidi usijikune, ogea maji ya baking soda au pakaa baking soda mwilini, “ imesema moja ya jumbe hizo katika mtandao wa X ikipendwa (like) na watu 329 kufikia Machi13, 2025.

Mgonjwa mwenye dalili za awali za Mpox au aliyekwisha kupata matibabu ya hospitali anaweza kutumia baking soda kuimarisha ngozi iliyoharibika na vipele vinavyotokana na ugonjwa huo lakini si kujitibu.Picha|India Times.
Ukweli huu hapa
Taarifa ya WHO iliyotolewa Septemba 2, 2022 inabainisha mbinu kadhaa unazoweza kutumia kukabiliana na vipele vinavyoambatana na ugonjwa huo baada ya kupata matibabu ya hospitali ikiwemo kuoga kwa kutumia baking soda na sio kuzitumia kama njia ya kujitibu.
“Jinsi ya kutunza vipele: Usijikune, osha mikono yako kabla na baada ya kugusa vidonda, weka vipele vyako vikiwa vikavu na usivifunike jisafishe kwa maji yaliyochemshwa au antiseptiki…
…Suuza vidonda vilivyo mdomoni kwa maji ya chumvi, oga kwa maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na baking soda au chumvi, tumia paracetamol kupunguza maumivu na usumbufu wa vidonda,” umesema mwongozo wa WHO.
Pamoja na hayo, WHO na Wizara ya Afya inabainisha kuwa mpaka sasa hakuna tiba kamili ya ugonjwa huo ila unaweza kupata matibabu kulingana na dalili husika ukitembelea vituo vya afya na sio kujitibu nyumbani kama ilivyoainishwa na watumiaji hao wa mitandao ya kijamii
“Kwa kuzingatia kuwa magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi hayana tiba mahususi ila mgonjwa anahudumiwa kulingana na dalili alizonazo. Hivyo Wizara inawasihi na kuwasisitiza wananchi wote kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga,” imesema taarifa ya Wizara hiyo ya Machi 10 mwaka huu.

Ufahamu ugonjwa wa Mpox
Kwa mujibu wa WHO, Mpox (monkeypox) ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya monkeypox (MPXV) ambavyo ni virusi vya jinsi ya Orthopoxvirus.
Ugonjwa huu huathiri binadamu na wanyama kama vile nyani, panya, paka, mbwa.
Dalili za Mpox zinaweza kujitokeza kati ya siku moja hadi 21 baada ya kuambukizwa na mara nyingi hudumu kwa wiki mbili hadi nne.
Dalili hizo ni pamoja na upele unaojitokeza na baadae kuwa vidonda, homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, uchovu na kuvimba kwa tezi za mwili.
Mpox huambukizwa kwa kugusa vidonda vya ngozi vya mtu aliyeambukizwa, kubusiana, kufanya ngono, kushika nguo au mate ya mtu mwenye maambukizi.
Latest



