Wagonjwa wa monkeypox wazidi kuongezeka
Vidonda vya monkeypox kwa kawaida vinapatikana kwenye viganja vya mkono. Picha| CDC.
- Sasa ni zaidi ya 550 duniani kote.
- Nchi 30 zaripoti wagonjwa hao huku nyingi zikiwa Afrika.
- WHO yabuni chanjo kuudhibiti usienee zaidi.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema zaidi ya watu 550 katika nchi 30 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa monkeypox ambao huenezwa na virusi vinavyofanana na vile vya ugonjwa wa ndui.
Nchi hizo 30 ni zile ambazo si kawaida kupata ugonjwa wa monkeypox.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema uchunguzi unaendelea lakini kuibuka ghafla kwa ugonjwa huu katika nchi hizo tena kwa wakati mmoja kunadokeza kuwa ugonjwa huo umekuweko muda mrefu bila kufahamika.
“Hadi sasa wagonjwa waliothibitishwa ni wanaume ambao wanajamiiana na wanaume wenzao,” amesema Mkuu huyo wa WHO akiongeza kuwa wagonjwa hao walifika katika kliniki za afya za masuala ya kujamiiana.
Kwa sasa amesema jamii hizo zinashirikiana kupasha habari watu wengine kuhusu hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo na kuchukua hatua kujikinga.
“Hata hivyo sote lazima tushirikiane tupambane na unyanyapaa ambao si kwamba ni kosa, bali pia unaweza kuzuia wenye maambukizi ya monkeypox kuogopa kusaka matibabu na hivyo kufanya hali ya kuzuia ugonjwa huu kuwa ngumu zaidi,” amesisitiza Dk Tedros.
WHO kwa upande wake unasihi nchi kupanua wigo wa ufuatiliaji na kusaka wagonjwa katika jamii nzima.
“Mtu yeyote anaweza kuambukizwa monkeypox iwapo atakaribiana na mtu ambaye tayari ameambukizwa,” amesema kiongozi huyo.
Zinazohusiana:
- Ni uzushi: Huwezi kupata maambukizi ya Corona kwa kuchangia damu
- Ukweli kuhusu maiti kuambukiza Corona
Kwa mujibu wa WHO, mlipuko huu wa monkeypox unasambazwa hasa kwa mgusano wa karibu wa ngozi kwa ngozi, ingawa virusi hivyo vinaweza pia kupitishwa na matone ya kupumua na matandiko machafu.
Kipindi cha virusi kuwepo mwilini kabla ya dalili kwa kawaida ni kuanzia siku sita hadi 13 lakini kinaweza kuanzia siku tano hadi 21.
Dalili zinaweza kuwa sawa na zile zinazowapata wagonjwa wa ndui, ingawa si mbaya sana kiafya, lakini huambatana na vipele na homa.
WHO inafanya nini?
Ingawa dalili za Monkeypox hupotea zenyewe, WHO inaonya kuwa kwa baadhi ya wagonjwa hali inaweza kuwa mbaya ambapo linaendelea kupokea taarifa za milipuko ya ugonjwa huo barani Afrika ambako ugonjwa huo umejikita.
Kipaumbele cha sasa ni kutoa taarifa sahihi kwa makundi yaliyo hatarini kuambukizwa, kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo miongoni mwa makundi hatarini, kulinda wahudumu wa afya walio mstari wa mbele na kuongeza uelewa zaidi kuhusu ugonjwa wa ugonjwa huo.
Chanjo zilizotumika wakati wa kutokomeza ndui, zilitoa pia kinga dhidi ya Monkeypox. Hata hivyo, chanjo mpya zimebuniwa na moja imethibitishwa kukinga ugonjwa huo.
Latest