Serikali yatoa mwongozo kwa wasafiri kudhibiti M-Pox

March 12, 2025 12:29 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasafiri watakiwa kuchukua tahadhari ikiwemo kutakasa mikono na kuripoti mto yoyote mwenye dalili za ugonjwa huo.

Arusha. Serikali ya Tanzania imetoa mwongozo kwa wasafiri wa safari za ndani na nje ya nchi utakaosaidia kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Nyani(M- Pox )na kuzuia kusambaa katika maeneo mengine.

Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Monkeypox ambao ulitangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama dharura ya Afya ya Kimataifa (PHEIC) mnamo Agosti 2024. 

Muongozo huo unakuja ikiwa ni siku mbili tangu Wizara ya Afya itangaze wahisiwa wawili kuthibitika kuathirika na ugonjwa huo nchini baada ya uchunguzi wa kitabibu.

Taarifa ya Seif Shekilage, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya iliyotolewa Machi12, 2025 inabainisha kuwa mwongozo huo utaanza kufanya kazi mara moja ukihusisha uchukuaji wa hatua madhubuti ikiwemo wafanyakazi na wasafiri kuzingatia usafi wa mikono na kupeana  nafasi kwenye mikusanyiko.

“Wasafiri na wafanyakazi wote katika maeneo ya mipakani wanapaswa kuzingatia hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kama vile unawaji wa mikono, kuacha angalau umbali wa mita moja baina ya mtu mmoja na mwingine…

….kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa kwa kupiga simu namba 199 bure, kutoa taarifa ofisi ya afya mipakani au kituo cha afya kilicho karibu,” imesema taarifa ya Shekilagii.

Mwongozo huo pia umeelekeza maeneo yote ya mipaka (viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari), wasafiri wote kufanyiwa uchunguzi wa awali wa afya ikiwamo kupimwa joto la mwili na watakaobainika kuwa na homa na au vipele watafanyiwa uchunguzi wa kina wa kiafya.

Pia Wizara ya Afya imesema itatoa elimu kuhusu utoaji wa taarifa mapema na ushauri wa afya kuhusu kuripoti dalili zozote za ugonjwa wa Mpox kwa wasafiri wote mipakani na wale watakaoonesha dalili hizo watafanyiwa uchunguzi wa kina na kupatiwa matibabu katika vituo vya huduma za afya huku waliohusina na wagonjwa kufualiwa afya zao.

“Watu wote waliotangamana na wagonjwa wa Mpox watashauriwa kufuatilia afya zao na kutoa taarifa katika kituo cha afya kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bure iwapo watakuwa na dalili zozote za Mpox,” imesema taarifa ya Shekilagi.

Aidha, wasimamizi na wamiliki wote wa vyombo vya usafiri pamoja na madereva wanapaswa kufuata taratibu za kiafya ikiwamo uchunguzi wa afya, ukaguzi wa usafi wa vyombo vya usafiri, usafi binafsi na kutoa taarifa kuhusu msafiri yeyote mwenye dalili za Mpox kwa mamlaka za afya mipakani.

Pamoja na tahadhari hiyo kwa wasafiri wa ndani na nje ya nchi tayari baadhi ya taasisi ikiwemo za kidini zimeanza kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo ikiwemo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) lililotoa utaratibu wa misa zake ikiwemo kusitisha kupeana amani kwa mikono.

Jumanne, Machi 11, 2025, Mkuu wa Idara ya Liturujia wa TEC, Padri Clement Kihiyo ametoa taarifa fupi akisema “Wapendwa katika Kristo,

kutokana na tahadhari ya kiafya iliyotangazwa na Wizara ya Afya, kwa upande wa Liturujia tunasitisha kwa muda maji ya baraka kwa kuchovya hadi hali itakapotengemaa,”.

Hatua hiyo inalenga kuwalinda waumini hao na ugonjwa huo ambao pamoja na visababishi vingine unasambaa kwa njia ya kugusana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks