Ukame kuchochea migogoro ya binadamu, wanyamapori Tanzania

September 10, 2020 12:22 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakati wa msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba – Disemba 2020, maeneo mengi ya nchi yatakuwa na  vipindi virefu vya ukavu.
  • Hali hiyo itachangia upungufu mkubwa wa malisho na maji kwa wanyamapori katika mbuga na kusababisha migogoro na binadamu.
  • TMA yashauri hatua stahiki za maandalizi na mbinu za kukabiliana na upungufu wa mvua. 

Dar es Salaam. Huenda migogoro ya wanyamapori na wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa ikaongezeka nchini baada watalaam wa hali ya hewa kutabiri kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kutakuwa na upungufu wa malisho na maji kwa wanyamapori. 

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), athari hizo zinaweza kutokea endapo kutakuwa na upungufu wa mvua za vuli zitakazonyesha mwezi Oktoba hadi Desemba 2020 katika mikoa inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka ikiwemo Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. 

Taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba – Disemba 2020 ya TMA inaeleza kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani (za kawaida) na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema kutokana na hali hiyo ya ukavu, kutakuwa na upungufu mkubwa wa malisho na maji kwa wanyamapori katika mbuga ambao unaweza kusababisha migogoro kati ya sekta husika na jamii wakati wanyamapori wanapotafuta malisho na maji. 

“Aidha, kuna uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kwa wanyamapori kutokana na ukosefu wa malisho na maji,” amesema Dk Kijazi katika taarifa hiyo iliyotolewa Septemba 8, 2020.  

Mtaalamu huyo amebainisha kuwa hali ya hewa inayotarajiwa, inaweza kusababisha magonjwa ya wanyamapori kusambaa kwa wanyama wanaofugwa kutokana na wanyamapori kuingia katika makazi ya jamii zinazozunguka hifadhi na mbuga. 

Katika baadhi ya hifadhi ya Taifa ikiwemo ya Nyerere iliyopo Rufiji mkoani Pwani, tembo wamekuwa wakivamia na kuharibu makazi na mashamba ya wakulima wanaoishi karibu na hifadhi hiyo. 

TMA imeeleza kuwa, kuna uwezekano wa kutokea matukio ya moto katika mapori na misitu katika maeneo hayo. hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati thabiti ya kukabiliana na hali hiyo. 

Kwa mujibu wa TMA, Hali ya joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki ya bahari ya Pasifiki liko chini ya wastani na inatarajiwa kuendelea kuwa hivyo katika kipindi chote cha msimu wa Oktoba hadi Disemba 2020. 

Hali hiyo inatarajiwa kupunguza nguvu ya mifumo inayosababisha mvua katika maeneo mengi yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka hapa nchini. 


Soma zaidi:


Naye Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dk Iddi Lipende anasema wanyamapori wana mapitio yao ya asili (shoroba) ambayo wanayatumia kupita kutoka sehemu moja kwenda nyingine kizazi hadi kizazi hata kama kuna makazi ya watu au mashamba.

Anasema hali hiyo pia husababisha migogoro ya tembo na binadamu na hivyo kuwaletea madhara kwa sababu wanyama hao wanakariri njia za kupita na hawawezi kubadilisha.

“Hata ukilima katika njia zao watapita tu kwa sababu wamezoea na wataleta madhara. Binadamu wanatakiwa kufahamu tabia za wanyama hawa ili kuepuka migogoro,” anasema Dk Lipende wakati akizungumza na Nukta hivi karibuni. 

Nini kifanyike?

Dk Kijazi amesema hatua stahiki za maandalizi na mbinu za kukabiliana na upungufu wa mvua ziendelee kuchukuliwa ili kupunguza migogoro hiyo. 

“Mamlaka husika zinashauriwa ziendelee kutoa elimu kwa jamii husika. Aidha, jamii inayozunguka mbuga itoe taarifa mapema kwa sekta ya wanyamapori pindi wanyama wanapokuwa wameingia katika maeneo yao,” amependekeza Dk Kijazi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dk Stephen Nindi ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa Serikali iko katika mchakato wa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi kwa jamii zote zinazozunguka hifadhi za Taifa ili kuondoa migogoro ya wanyamapori na binadamu ikiwemo uvamizi unaofanywa na tembo kwenye mashamba ya wakulima.

“Mpango huu utazingatia mambo mengi ikiwemo ikolojia ya wanyama na rasilimali za vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kuhakikisha ardhi inatumiwa vizuri na kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika,” anasema Dk Nindi.

Mvua za vuli zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV