Ujio mvua za vuli: Wakulima, wavuvi watahadharishwa Tanzania
- Mvua hizo zitanyesha mwezi Oktoba hadi Disemba 2020 katika maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka.
- Mvua hizo zitakuwa chache na zinaweza kusababisha ukame na upungufu wa maji.
- Wakulima, wafugaji watakiwa kuchukua hatua kupunguza athari za hali hiyo katika uzalishaji wa mazao.
Dar es Salaam. Wakulima, wavuvi na wafugaji wanaoendesha shughuli zao katika mikoa ya Tanzania inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka wametakiwa kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwemo kuzalisha mazao yanayokomaa kwa muda mfupi kutokana na uwezekano wa kupungua kwa mvua katika maeneo yao.
Mvua hizo ni za msimu wa mvua za vuli ambazo zitanyesha mwezi Oktoba hadi Disemba 2020 katika mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja, Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba – Disemba 2020 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaeleza kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani (za kawaida) na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.
“Mvua za vuli zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020,” inaeleza taarifa hiyo ya TMA iliyotolewa Septemba 9, 2020.
Licha ya kuwa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache.
Mambo ya kuzingatia kwa wakulima, wavuvi na wafugaji
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema katika kipindi hicho kunatarajia kuwepo kwa upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na visumbufu vya mazao na magonjwa vinatarajiwa kuongezeka.
Dk Kijazi amesema hali hiyo inatarajiwa kusababisha ukuaji hafifu wa mazao jambo linaloweza kuathiri mwenendo wa uzalishaji na masoko ya wakulima.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, TMA imewataka wakulima kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa ndani ya muda mfupi na kutumia teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi unyevunyevu na maji.
“Wakulima wanashauriwa kupata ushauri kutoka kwa maafisa ugani juu ya namna bora ya kuendesha kilimo kwa usalama wa chakula na lishe,” amesema Dk Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (IMO).
Kwa upande wa mifugo na uvuvi, hali ya kupungua kwa magonjwa ya mifugo na mazao ya uvuvi kama samaki na mwani inatarajiwa kwa sababu ya mtiririko hafifu wa maji utakaosababisha uzalishaji mdogo wa mazao ya samaki na mifugo.
Aidha, bosi huyo amesema kutokana na upungufu wa malisho na maji kuna uwezekano wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji kujitokeza katika kipindi hicho cha mvua za vuli.
“Wafugaji na wavuvi wanashauriwa watumie utabiri wa hali ya hewa na kufuata ushauri wa maafisa ugani,” amesema Dk Kijazi.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini
Nini kitasababisha mvua kupungua?
Kwa mujibu wa TMA, Hali ya joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki ya bahari ya Pasifiki liko chini ya wastani na inatarajiwa kuendelea kuwa hivyo katika kipindi chote cha msimu wa Oktoba hadi Disemba 2020.
Hali hiyo inatarajiwa kupunguza nguvu ya mifumo inayosababisha mvua katika maeneo mengi yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka hapa nchini.
Pia joto la bahari la wastani linatarajiwa katika maeneo ya upande wa magharibi mwa Bahari ya Hindi wakati upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi unatarajiwa kuwa na joto la bahari la juu ya wastani.
“Hali hii inatarajiwa kupunguza msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka baharini kuelekea katika maeneo ya pwani na nyanda za juu kaskazini mashariki mwa nchi,” inaeleza taarifa ya uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa ya TMA.
Aidha, joto la wastani hadi juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya kusini-mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (karibu na pwani ya Angola) ambapo itaendelea wakati wa vuli na kupunguza msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo mengi nchini.
Kutokana na mifumo hiyo ya hali ya hewa, maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka yatakuwa na ukavu na hivyo kuathiri shughuli mbalimbali.