Mfahamu mwanamke aliyeaminiwa kuandika historia mpya ya TBC

July 15, 2026 4:04 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Asha Dachi Mbaruk, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). 
  • Anakua mwanamke wa kwanza kuiongoza TBC tangu ilipoanzishwa 2007.
  • Anatarajiwa kuliimarisha shirika hilo kutokana na uzoefu wake wa uongozi. 

Dar es Salaam. Uteuzi wake umebeba ujumbe mzito kuliko cheo chenyewe. Ameaminiwa kuongoza moja ya taasisi kubwa ya habari nchini. 

Ni Asha Dachi Mbaruk, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). 

Rais Samia amemteua Asha katika nafasi hiyo jana Julai 14, 2026. Kabla ya uteuzi huo, Asha alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Ayub Rioba ambaye amemaliza muda wake. 

Kwa baadhi ilikuwa ni taarifa ya kawaida ya uteuzi, lakini kwa wadau wa tasnia ya habari ni tofauti. Ni uteuzi unamfikisha kileleni mtendaji ambaye kwa miaka ya hivi karibuni ameaminiwa kuongoza taasisi kubwa za habari za Serikali. 

Mbaruk anakabidhiwa TBC katika kipindi ambacho sekta ya utangazaji inapitia mageuzi makubwa ya teknolojia kuliko wakati mwingine wowote. 

Kuongezeka kwa ushindani kutoka majukwaa ya kidijitali, mabadiliko ya tabia za watazamaji na wasikilizaji, pamoja na kasi ya maendeleo ya teknolojia ambayo yamekuwa yakitishia uhai wa vyombo vya habari vya asili. 

Safari iliyoanzia ndani ya TBC

Tofauti na viongozi wanaoingia TBC kutoka taasisi nyingine, Asha si mgeni ndani ya shirika hilo. 

Kabla ya kurejea kama Mkurugenzi Mkuu, aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Redio, nafasi iliyompa fursa ya kuelewa kwa karibu mifumo ya uendeshaji wa shirika pamoja na majukumu ya utangazaji wa umma.

Uzoefu huo ulimjengea msingi wa uongozi ambao baadaye ulimpeleka katika taasisi nyingine muhimu ya habari.

Mwaka 2024, Serikali ilimhamishia TSN, kampuni inayochapisha magazeti ya Serikali ikiwemo Daily News, Sunday News, HabariLEO na SpotiLEO.

Aliteuliwa kwanza kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, kabla ya kuthibitishwa rasmi na Rais Samia kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TSN  Oktoba 31, 2024.

Akiwa TSN alionyesha ubobevu wa uongozi kwa kusimamia utendaji makini wa kampuni hiyo ambayo mwaka huu imepata tuzo ya Chombo Bora Cha Habari cha Serikali Kinachotii Sheria Zaidi 2025.

Utendaji mzuri wa kuongoza TSN chini ya kipindi cha miaka miwili, umekuwa tiketi ya kupelekwa katika daraja la juu la kuiongoza TBC huku akiungana na wanawake wachache wanaoshikilia nafasi za juu za uongozi katika sekta ya habari Tanzania.

Wanawake wengine ni Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia. 

Anakuwa mkurugenzi mkuu wa nne wa TBC

Asha anakua mkurugenzi mkuu wa nne wa TBC tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.

Historia ya shirika hilo ilianza baada ya Serikali kuunganisha Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na Television ya Taifa (TVT) ili kuunda chombo kimoja cha utangazaji wa umma.

Mkurugenzi Mkuu wa kwanza alikuwa Tido Mhando aliyeteuliwa mwaka 2006 wakati wa maandalizi ya kuanzishwa kwa shirika hilo. Baada ya TBC kuzinduliwa rasmi mwaka 2007, aliendelea kuiongoza huku akisimamia ujenzi wa mfumo mpya wa utangazaji uliounganisha redio na televisheni chini ya taasisi moja.

Mhando aliyekuwa mtendaji mkuu wa kampuni ya Azam Media kwa sasa ni mshauri wa Rais Samia wa masuala ya habari na mawasiliano.

Aprili 27, 2011, uongozi ukahamia kwa Clement Mshana, ambaye kabla yake alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo). Katika kipindi chake cha takribani miaka mitano, Mshana alisimamia kuimarishwa kwa taasisi hiyo baada ya kipindi cha mpito cha kuanzishwa kwake.

Machi 2016, Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli, alimteua Dk Rioba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC. 

Kwa karibu muongo mmoja, Rioba aliongoza shirika hilo katika kipindi kilichoshuhudia kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kidijitali na kupanuka kwa huduma za redio na televisheni za TBC.

Historia yake bado inaandikwa

Asha amepewa jukumu muhimu la kusimamia taasisi yenye historia ya zaidi ya nusu karne ya utangazaji wa umma nchini, kuanzia enzi za Sauti ya Dar es Salaam, baadaye Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), hadi kuundwa kwa TBC mwaka 2007.

Tofauti na viongozi wengine wanaojulikana kwa wasifu mpana, taarifa nyingi kuhusu Asha bado hazijawekwa wazi hadharani. Hata hivyo, safari yake ya kitaaluma inatosha kuelezea kwa nini ameendelea kuaminiwa.

Asha anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza TBC tangu kuanzishwa kwake takriban miaka 20 iliyopita. Jina lake halitaingia tu kwenye orodha ya wakurugenzi wakuu wa shirika hilo, pia katika historia ya mageuzi ya uongozi wa taasisi za habari nchini. 

Changamoto iliyo mbele yake si kufika kileleni, bali kuandika urithi ambao utaifanya Julai 14, 2026 ikumbukwe kama mwanzo wa enzi mpya ya TBC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jul, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Nukta TV

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Nukta TV

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Nukta TV