TTCL yaanza kuleta ushindani huduma za kifedha Tanzania

June 4, 2022 10:33 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ndani ya mwaka mmoja TTCL imeongeza watumiaji wa T-Pesa hadi kumiliki asilimia 4 ya soko kutoka asilimia 2 mwaka 2021. 
  • Watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu wazidi kuongezeka kwa kasi.
  • Vodacom, Airtel na Tigo zaendelea kutawala soko la huduma za kifedha kwa njia ya simu.

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya TTCL imeendelea kutoa ushindani katika soko la mawasiliano Tanzania kwa kuongeza watumiaji wake wa huduma za kifedha kwa njia ya simu huku ikimiliki asilimia nne ya soko la huduma hizo.

Kwa mujibu wa takwimu za mawasiliano za robo ya kwanza ya mwaka 2022 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivi karibuni, hadi kufikia Machi2022, watumiaji wa huduma za kifedha za TTCL (T-Pesa) walikuwa milioni 1.4 kutoka 762,196 kipindi kama hicho mwaka 2021. 

Idadi hiyo ya wateja wa T-Pesa waliorekodiwa Machi mwaka huu sawa na asilimia nne ya soko lote la huduma za kifedha nchini Tanzania.

Umiliki wa T-Pesa katika soko la huduma za kifedha kwa njia ya simu Tanzania umechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji ambapo wameongezeka kwa asilimia 44.8 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Idadi hiyo ya watumiaji T-Pesa ni sawa na asilimia 77.7 (takriban watumiaji nane kati ya 10) ya watumiaji milioni 1.8 wa mtandao wa mawasiliano wa TTCL ambao walikuwa wamesajiliwa hadi Machi mwaka huu.

Mafanikio hayo ya TTCL yanatokana na uwekezaji na uwezeshaji unaofanywa na Serikali kuiboresha kampuni hiyo ya umma kutoka katika mifumo ya analojia kwenda dijitali ili kutoa ushindani katika soko la mawasiliano Tanzania.

 

TTCL bado ina kibarua kigumu

Hata hivyo, T-Pesa bado ina kibarua kigumu cha kuendelea kuongeza watumiaji wake wa huduma za kifedha ikizingatiwa kuwa inashindana na kumpuni kama Vodacom, Airtel na Tigo ambazo kwa pamoja zinamiliki zaidi ya asilimia 80 ya soko hilo.

Kwa sasa, M-Pesa ya Vodacom ndiyo kinara wa soko la huduma za kifedha kwa njia ya simu nchini ambayo hadi Machi mwaka huu ilikuwa na watumiaji milioni 14.2 sawa na asilimia 40 ya watumiaji wote Tanzania.

Hata hivyo, kiwango cha umiliki wa soko cha M-Pesa kimeshuka kutoka asilimia 42 ya Machi 2022 licha ya kuwa watumiaji wake wameongezeka. 


Soma zaidi:


Mchuano bado mkali

Kwa mujibu wa TCRA, watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu Tanzania hadi kufikia Machi mwaka huu walikuwa milioni 35.7 wakiongezeka kutoka milioni 32.7 waliokuwepo mwaka mmoja uliopita ambao unaishia Machi.

Licha ya watumiaji wa huduma hizo kuongezeka, mchuano unabaki kwa vinara watatu ambao ni M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money ambao wote kwa pamoja wanamiliki asilimia 87 ya soko lote.

Huduma za kifedha kwa njia ya simu  za mkononi zimekuwa mkombozi katika nchi zinazoendelea katika kurahisisha miamala ya kifedha katika maeneo ambayo hakuna huduma za benki. 

Miongoni mwa huduma zinazotumika zaidi kupitia simu za mkononi ni pamoja na kutuma na kupokea pesa, mikopo midogo midogo, bima, na huduma za akiba jambo linaloongeza ujumuishi katika huduma za kifedha Tanzania. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW