Vodacom, Tigo: Jino kwa jino watumiaji wa simu Tanzania
- Hadi kufikia Machi, 2022 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu milioni 55.4
- Vodacom, Airtel zachuana vikali kupata wateja.
- Wadau wasema simu ni fursa ya kuboresha maisha, biashara.
Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa simu za mkononi imeongezeka kwa asilimia 4.9 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja huku ushindani mkali ukionekana zaidi kwa kampuni za Vodacom, Tigo na Airtel zinazotoa huduma hiyo ya mawasiliano Tanzania.
Matumizi ya simu hupimwa kwa idadi ya watu waliojisajili kutumia mitandao ya simu za mkononi inayotoa huduma hiyo nchini ikiwemo ya Vodacom, Tigo, TTCL, Zantel, Halotel na Smile.
Uchambuzi wa takwimu za robo ya kwanza ya mwaka 2022 (Januari-Machi 2022) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa simu imeongezeka kutoka watumiaji milioni 52.8 waliokuwepo Machi mwaka jana hadi milioni 55.4 waliorekodiwa Machi mwaka huu.
Hiyo ni sawa na ongezeko la watumiaji milioni 2.6 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaoishia mwezi Machi.
Ni ushindani
Licha ya idadi ya watumiaji wa simu kuongezeka kila mwaka nchini, mtandao wa Vodacom ndiyo unaongoza kuwa na watumiaji wengi, jambo linalotoa ushindani mkali kwa kampuni nyingine.
Hadi kufikia Machi 2022, Vodacom ilikuwa na watumiaji milioni 16.7 sawa na asilimia 30.1 ya watumiaji wote simu za mkononi.
Hiyo ni sawa na kusema kwa kila watumiaji 10 wa simu Tanzania, watatu wanatumia mtandao wa Vodacom kupata mawasiliano ya simu.
Vodacom inachuana vikali na Tigo na Airtel ambapo kampuni zote tatu zinaunda asilimia 83.7 ya soko lote la watumiaji wa simu Tanzania.
Tigo inashika nafasi ya pili kwa kuwa na watumiaji wa simu za mkononi kwa watumiaji milioni 14.8 ikifuatiwa kwa karibu na Airtel ambayo imesajili watumiaji milioni 14.7.
Wakati Vodacom ikiongoza kwa watumiaji wengi wa simu za mkononi Tanzania, mtandao wa Smile una watumiaji wachache zaidi wanaofikia 12,704 au sawa na asilimia 0.02 ya watumiaji wote.
Juu ya Smile yuko TTCL ambaye ana watumiaji milioni 1.8 na idadi yake imekuwa ikiongezeka kwa taratibu licha ya kampuni hiyo ya Serikali kufanyiwa mabadiliko mbalimbali ya uendeshaji na uwezeshaji ili iweze kutoa ushindani katika soko la mawasiliano ya simu za mkononi Tanzania.
Simu ni kifaa muhimu ambacho katika kipindi hiki cha mapinduzi ya kidijitali kimekuwa kiungo muhimu cha mawasiliano ya watu na biashara mbalimbali zinazofanyika kwa njia ya kawaida na mtandaoni kwa sababu utendaji wake hauingiliwi na mipaka ya jiografia.
Wengi wanatumia simu za kawaida
Licha ya idadi ya watumiaji wa simu za mkononi kuongezeka kila mwaka, idadi kubwa wanatumia simu za kawaida ambazo hazijaunganishwa na intaneti, jambo ambalo linawazuia kufaidika na fursa za mtandaoni ikiwemo biashara, ajira na mafunzo na elimu.
Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema ni asilimia 27 tu ya Watanzania ndiyo wanatumia simu janja (smartphone) kwa sababu gharama za juu kuzipata simu hizo ambazo wengi hawawezi kuzimudu.
“Eneo ambalo tulitamani kama Serikali kupata wawekezaji ni eneo la upatikanaji wa simu janja (smartphones na tablets) ili ziwe bei nafuu na watu waweze kumudu kununua,” alisema Nape Mei 26, 2022 jijini Dar es Salaam alipokutana na Katibu wa Mambo ya Nje wa Canada, Robert Oliphant.
Nape alisema kuongeza idadi ya watumiaji wa simu janja, wawekezaji wajenge viwanda vya bidhaa hiyo nchini na kuziuza kwa bei nafuu.
Zinazohusiana:
- Matumaini makubwa kuzaliwa mji wa Silicon Dar
- Apple waingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Makumbusho inavyogeuka Kariakoo ndogo ya simu za mkononi Dar
Ni fursa kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa simu
Kwa mujibu wa ripoti ya mapinduzi ya kidijitali ya mwaka 2019 ya GSMA, ongezeko la matumizi ya simu linasaidia kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi.
Ripoti hiyo inaeleza pia kuwa teknolojia ya simu za mkononi inatumika kama jukwaa la kuboresha huduma za afya, elimu, biashara, upashanaji habari, ajira na uvumbuzi.
“Hii inaongeza kipimo cha kiuchumi, kijamii na thamani ya kitamaduni, kutokana na kuboresha tija na ufanisi katika shughuli za sekta za uchumi, ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kuboresha maisha kwa watu na jamii,” imeeleza ripoti hiyo.
Mtaalam wa kujitegemea wa programu za kompyuta, Sogwejo Kaboda amesema kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa simu nchini ni kiashiria kuwa Watanzania wameona umuhimu wa kutumia teknolojia katika kufanikisha shughuli zao za maendeleo.
“Simu zinarahisisha mambo mengi ikiwemo kuokoa muda ambao wanautumika katika shughuli za uzalishaji mali. Pia ni fursa ya kuboresha maisha kwa sababu zinawaunganisha na fursa mbalimbali za kibiashara,” amesema Kaboda wakati akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Latest



