Watumiaji simu benki wazidi kuongezeka Tanzania, wafikia milioni 32.7
- Idadi hiyo imeongezeka kutoka watumiaji milioni 32.5 mwezi Januari mwaka huu.
- Vodacom inaongoza kwa kuwa na wateja wengi kwa asilimia 42.
Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi inazidi kupaa kwa kasi nchini Tanzania baada ya kufikia milioni 32.7 mwezi Machi mwaka huu.
Kwa mujibu Takwimu mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Machi 2021 (robo ya kwanza ya mwaka huu) watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi Tanzania wafikia milioni 32.7 ambapo wameongezeka kutoka milioni 32.5 mwezi Januari mwaka huu.
Hilo ni sawa na ongezeko la watumiaji 298,346 (asilimia 0.9) ndani ya kipindi cha miezi mitatu huku idadi hiyo ikiongezeka kila mwezi.
Watumiaji wa huduma za kibenki Tanzania wamekuwa wakiongezeka kwa kasi. Mfano, Desemba mwaka jana kulikuwa na akaunti za simu benki (mobile money subscribers) milioni 32.26 milioni zilizokuwa zimeongezeka kwa kasi kutoka akaunti takriban milioni 31.1 mwishoni mwa Oktoba 2020.
Wadau wa masuala ya uchumi na fedha wanaeleza kuwa takwimu hizo zinadhihirisha kuwa Watanzania wengi wanazidi kufikiwa na huduma za kifedha na kuchangia katika ukuaji wa uchumi kwa kuiwezesha Serikali kupata mapato.
Katika takwimu hizo za TCRA zilizotolewa wiki hii, zinabainisha kuwa asilimia 88 ya watumiaji wote wa huduma za kifedha kwa njia za simu wanatumia M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel.
Kampuni tatu zilizosalia za Zantel inayoendesha huduma ya Eazy Pesa, Halotel (Halopesa) na TTCL (TTCL Pesa) zilizosalia zinagawana asilimia 12 ya watumiaji hao wa huduma za kifedha.
Katika mchuano huo, M-pesa ndiyo inayotawala soko nchini baada ya kuweka kurekodi watumiaji milioni 13.6 sawa na asilimia 42 ya soko zima ikifuatiwa na Tigo Pesa (asilimia 26) na Airtel Money ikiwa na asilimia 20.
Vodacom kupitia M-Pesa imezidi kuongeza wateja wake, licha ya ushindani mkali baada ya takwimu hizo mpya kuonyesha kuwa ilivuna watumiaji zaidi ya 517,443 ndani ya miezi mitatu kutoka watumiaji milioni 13.2 Januari 2021.
Huduma za kifedha kwa njia ya simu zinawawezesha watu kufanya miamala mbalimbali na hivyo kuokoa muda na gharama za kwenda benki jambo linalorahisisha utendaji wa biashara na shughuli mbalimbali za kijamii.
Mtaalam wa kujitegemea wa masuala ya mahusiano ya umma na masoko ya mtandaoni, Godfrey Kijanga amesema kuongezeka kwa watumiaji huduma za kifedha kwa njia ya simu ni ishara kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya masuala ya fedha jumuishi na kuwapatia fursa ya kufanya vitu vingi mtandaoni.
Amesema matumizi ya huduma yanazidi kuwarahishia Watanzania maisha na kuwafungulia fursa nyingi za kibiashara kwa sababu mzunguko wa fedha umerahisishwa na wanaweza kufanya miamala popote walipo.
“Kwa sasa ukitoka nje utakutana na kibanda kinachotoa huduma za kifedha na anaweza kufanya miamala hata akiwa ndani na kufanikisha mambo yako kwa haraka,” Kijanga ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Soma zaidi:
- Watumiaji wa huduma za simu benki wazidi kupaa Tanzania, wafikia milioni 23
-
Miamala ya kifedha simu za mkononi yafikia Sh7.8 trilioni kwa mwezi Tanzania
Aidha, Kijanga aliyewahi kuwa Afisa Mahusiano wa soko la mtandaoni la Jumia Tanzania amesema ongezeko la watumiaji wa huduma hizo pia linaibua changamoto katika sekta ya benki nchini kwa sababu idadi ya watu wanaokwenda benki inapungua.
Amesema mabadiliko hayo ya huduma za kifedha yawe chachu kwa wao kubuni na kuboresha zaidi huduma zao ili kuendeleza ushindani na kuwafikia wateja wanaotumia simu kupata huduma za kifedha.
“Zile safari za watu kwenda kwenye matawi ya benki zimepungua. Ni changamoto kwa mabenki wanatakiwa wajitafakari namna ya kuendana na mabadilio ya teknolojia kwa sababu kwa hatua tuliyofikia hatuwezi kuikwepa simu katika upatikanaji wa huduma za kifedha,” amesema Kijanga.