NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa

Zahara Tunda 0738Hrs   Agosti 24, 2018 Teknolojia
  • Kuwanufaisha watu wenye miamala zaidi ya mtandao mmoja wa simu.
  • Imebuniwa na vijana wa kitanzania.
  • HaIhitaji kuwa na mtandao wa intaneti ili Ifanye kazi.

Dar es Salaam. Umesahau neno la siri (Passward) ya mtandao wa simu au upoteza simu na huwezi tena kukamilisha miamala ya fedha kwa njia ya simu na hujui ufanye nini? 

Kwasasa itakuwa ni historia kwani vijana wa kitanzania wamegundua namna ya kukuwezesha kufanya miamala yote kwa kutumia programu ya simu (App) ukiwa popote bila kusubiri muunganiko wa mtandao wa intaneti au kupanga foleni benki na kwenye vibanda vya kutolea pesa. Pia inakuwezesha kulipia huduma za makampuni kwa kutumia simu yako ya kawaida au simu janja.

Yote hayo utayafanya kupitia App ya NALA  inayoendeshwa na vijana wa kitanzania wakiongozwa na Benjamin Fernandes; mshindi wa tuzo ya MBA World Summit na Mhitimu wa Shahada ya Umahili katika Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Stanford cha nchini Marekani.   

"Uhamishaji wa fedha kwa kutumia programu ya NALA ni rahisi mno ndani ya sekundi 10, muamala umekamilika na huhitaji kuwa na intaneti kukamilisha muamala huo," anaeleza Fernandes.

Kupitia NALA wateja wa mitandao ya Tigo, Airtel na Vodacom wanaweza kupokea na kutuma pesa bila kubadilisha laini ya simu au mchakato mrefu wa miamala.

“Ni App nzuri sana tunasubiri menu ya Halotel na TTCL,” anasema Francis Siza mtumiaji wa NALA.

Vilevile ni huduma nzuri ya kufuatilia mwenendo wa pesa zako, kufahamu taarifa ya kiasi ulichotoa na kupokea kwa wakati wote, “Ukiachana na muonekano wake mzuri, kitu kikubwa kuhusu NALA ni kwamba ni rahisi sana kutumia.” anasema Enock Mbise kutoka mkoa wa Tanga. 

App hiyo yenye wafuasi zaidi ya 40,000 itakuwezesha kulipia bili za LUKU na Dawasco bila kuingiza neno la siri mara kwa mara, hii ni kwasababu ukiweka kwa mara ya kwanza itahifadhiwa katika kumbukumbu na itakurahisishia kulipia tena bila kuwa na mawazo ya kufikiria kuandika tena neno la siri.  

Benjamin Fernandes, Mwazilishi wa NALA, akielezea jinsi inavyofanya kazi katika mkutano wa Mfumo wa Taifa wa Fedha Jumuishi akielezea kuhusu ubunifu katika kuendeleza mifumo ya benki Tanzania.Picha| Mtandao.

Ufanisi wa NALA umeifanya kukubalika zaidi na watu wengi ambapo hivi karibuni ilishika nafasi ya nne katika orodha za Apps za fedha nchini zenye umaarufu katika duka la Google (Play Store) na kukaa katika nafasi hiyo kwa siku 17 mfulululizo

Vilevile imefanikiwa kuingia katika shindano la Ecobank Fintech Challenge 2018 linalohusisha wabunifu wa teknolojia ya fedha kwa nchi za Afrika ikiwa katika 11 bora, ambapo kilele cha shindano hilo kitafanyika Lome, Togo na kama NALA itafanya vizuri inaweza kuibuka na kitita cha Dola za Marekani 10,000.  


Ulinzi wa namba zako za siri?

Hofu ya kuweka akaunti zako zote katika muamala mmoja inaibua changamoto lakini kwa kuligundua hili NALA wanahakikisha usalama wa pesa zako na malipo yoyote unayofanya yanahifadhiwa vizuri kwa viwango vya juu.

Teknolojia ya ulinzi wanayotumia ni inatumika na karibu benki 500 duniani katika kulinda miamala ya watu kwenye akaunti zao, vilevile ukiondoa namba za siri za kuchukulia pesa kwenye mitandao ya simu, NALA inakupa nafasi ya kujiwekea namba za siri ili kuzuia mtu mwingine asiingie katika app yako.

   Huduma mbalimbali za kifedha zinazopatikana NALA na jinsi utakavyoweza kufuatilia miamala yako yote uliyofanya kupitia. Picha| Google Store

Licha ya ubunifu wa kurahisisha huduma bado kuna changamoto hasa kwa wawekezaji wakubwa bado hawajitokezi kwa wingi katika kuwainua wajasiriamali wadogo kwenye ubunifu wa teknolojia.

Hivyo kilio kikubwa kwa NALA na wabunifu wengine ni kuona wawekezaji wanajitokeza kuinua biashara za wabunifu zinazofanywa na vijana.

"Ushauri wangu, kwa wajasiriamali wenzangu na mimi ni tuendelee kufuata tunachokipenda na tusikate tamaa," anasema Fernandes.

Watumiaji wa NALA sehemu mbalimbali waisifia huduma hiyo kwa kuleta ahueni hasa kwa wale wanaotumia simu zaidi ya moja na kufanya miamala mbalimbali.


Related Post