TCU yafungua dirisha la pili udahili vyuo vikuu
- Litakuwa wazi kuanzia leo Agosti 25 mpaka Septemba 6, 2023.
- Waombaji wakumbushwa kuzingatia taratibu na kuepuka matapeli.
Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2023/24 litakalokuwa wazi kuanzia leo Agosti 25 hadi Septemba 6, 2023.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa katika taarifa yake iliyotolewa leo Agosti 25, amebainisha kuwa waombaji ambao hawakutuma maombi au kutodahiliwa katika awamu ya kwanza, watumie dirisha la pili kutuma maombi katika vyuo wavipendavyo.
Aidha, Prof Kihampa amezielekeza taasisi za elimu ya juu kutangaza programu ambazo bado zina nafasi ili kutoa fursa kwa watu ambao hawakupata nafasi katika awamu ya kwanza.
“Waombaji wa vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyopo katika tovuti ya TCU,” amesema Kihampa.
Kihampa amesisitiza waombaji udahili kuzingatia utaratibu wa udahili awamu ya pili kama ulivyoainishwa katika tovuti ya TCU.
Soma zaidi
-
Ufaulu matokeo kidato cha sita 2023 waongezeka kiduchu
-
Matokeo kidato cha sita 2023 haya hapa
-
Shule 10 bora matokeo kidato cha sita 2023 Tanzania
Pia waombaji udahili wa shahada ya kwanza wamekumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.
“kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa,” imeeleza taarifa ya Kihampa.
TCU imewataka waombaji kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
Kufunguliwa kwa dirisha hilo kumekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya maombi ya kujiunga katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 116,133 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 80 vilivyoidhinishwa kudahili ambapo waombaji 86,624 sawa na asilimia 74.6 ya waliotuma maombi wameshapata udahili vyuoni.
“Mwenendo wa udahili wa Awamu ya Kwanza kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019 hadi 2023/2024) unaonesha ongezeko kubwa la waombaji ikiashiria ongezeko la wahitimu wa Kidato cha Sita na wale wa Stashahada,” amesema Prof Kihampa.