TCU yafungua awamu ya pili ya udahili vyuo vikuu Tanzania

September 3, 2024 2:53 pm · Mlelwa Kiwale
Share
Tweet
Copy Link
  • Dirisha kuwa wazi mpaka Septemba 21, 2024.
  • Waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja watakiwa kuthibitisha kuanzia leo.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza wa mwaka wa masomo 2024/2025 kwa siku 19 baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya udahili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TCU, Prof Charles Kihampa leo Septemba 3, 2024 udahili huo utaanza leo na kutamatika Septemba 21, 2024 ambapo waombaji ambao hawakupata nafasi ya kuomba udahili wa awamu ya kwanza wanahimizwa kutumia nafasi hiyo.

Kihampa amevitaka vyuo vya elimu ya juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi huku waombaji udahili na vyuo wakitakiwa kuzingatia utaratibu wa udahili wa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyoko katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).

Kwa mujibu wa Prof Kihampa katika awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 124,286 walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 86 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi katika shahada ya kwanza ambapo jumla ya programu 856 zimeruhusiwa kudahili ikilinganishwa na programu 809 mwaka 2023/2024.

“Vilevile kwa upande wa nafasi za udahili, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 198,986 ikilinganishwa na nafasi 186,289 mwaka uliopita. Hili ni ongezeko la nafasi 12,697 sawa na asilimia 6.8 katika programu za Shahada ya Kwanza,” amesema Prof Kihampa.

Aidha, jumla ya waombaji 98,890 sawa na asilimia 79.6 ya waombaji wote walioomba udahili katika awamu ya kwanza, wamepata udahili kwenye vyuo walivyoomba huku idadi ya waombaji wa udahili na watakaodahiliwa ikitarajiwa kuongezeka katika awamu zinazofuata.

Kwa waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo mpaka Septemba 3, 2024 ambapo uthibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili. 

Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.

Aidha, uthibitisho wa udahili unaweza kufanyika kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia wakati wa kuomba udahili ambapo kwa urahisi kurejea, orodha ya majina ya waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja inapatikana kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks