TCU yafungua dirisha awamu ya pili udahili vyuo vikuu
- Dirisha litakuwa wazi Agosti 24 hadi Septemba 6, 2021.
- Litawahusu waombaji wa kozi za shahada ya kwanza mwaka 2021/22.
- 68,019 wapata udahili awamu ya kwanza.
Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2021/22 litakalokuwa wazi kuanzia kesho.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa katika taarifa yake iliyotolewa leo Agosti 23, ameeleza kuwa Dirisha hilo litakuwa wazi Agosti 24 hadi Septemba 6, 2021.
Prof Kihampa amezielekeza taasisi za elimu ya juu kutangaza programu ambazo bado zina nafasi ili kutoa fursa kwa watu ambao hawakupata nafasi katika awamu ya kwanza.
“Waombaji wa vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyopo katika tovuti ya TCU,” amesema katibu mtendaji huyo.
TCU imesisitiza kuwa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakudahiliwa katika hawamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.
Pia waombaji udahili wa shahada ya kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.
“Pia kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha , vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa,” imeeleza taarifa ya Kihampa.
TCU imewataka waombaji kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
Kufunguliwa kwa dirisha hilo kumekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya maombi ya kujiunga katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 92,809 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 74 vilivyoidhinishwa kudahili ambapo waombaji 68,019 sawa na asilimia 73.2 ya wameshapata udahili vyuoni.
“Mwenendo wa udahili wa Awamu ya Kwanza kwa kipindi cha miaka minne (2018/2019 hadi 2021/2022) unaonesha ongezeko kubwa la waombaji ikiashiria ongezeko la wahitimu wa Kidato cha Sita na wale wa Stashahada,” amesema Prof Kihampa.
Habari hii imeandikwa na Medlini Kuya na Nuru Abdallah.
Latest
