Tanzania mwenyeji mkutano wa kimataifa wa utalii
- Ni mkutano wa kimtaifa utalii wa Shirika la Utalii Dunia (UNWTO).
- Utafanyika Arusha Oktoba mwaka huu.
- Utajadili namna ya kuimarisha sekta ya utalii Afrika.
Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimtaifa utalii wa Shirika la Utalii Dunia (UNWTO) Kamisheni ya Afrika ambao unalenga kujadili za namna ya kuiimarisha sekta ya utalii Afrika ili kuhimili majanga mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa Corona (Uviko-19).
Mkutano huo utakaofanyika jijini Arusha Oktoba 5 hadi 7, 2022 unatarajiwa kuhudhuriwa na mawaziri wa utalii a uhifadhi wanachama wa UNWTO na kufuatiwa na jukwaa la wazi kujadili kwa kina na kutoka na mapendekezo ya namna ya kujenga upya ustahimilivu wa utalii wa Afrika kwa maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi.
Huenda mapendekezo hayo yakasaidia kuimarisha sekta ya utalii Afrika kwa kuongeza idadi ya watalii na mapato baada ya Uviko-19, igonjwa ambao uliwafanya watu wengi kukosa kazi na kupungua kwa uhifadhi wa maliasili na bidhaa zinazotumika katika utalii.
Ili kufanikisha mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Francis Michael amezinduwa rasmi kamati ya kitaifa ya maandalizi ya mkutano huo wa 65 (65th UNWTO-CAF MEETING).
“Nategemea kamati hii itafanya kazi kwa weredi, maarifa na kuwa na kasi kubwa katika maandalizi haya,” amesema Dk Michael.
Amesema yupo tayari kushirikiana na kamati hiyo ili Tanzania iwe mfano kwa nchi nyingine wananchama wa umoja huu.
“Nina nafasi ya kufanya mabadiliko ya wajumbe wakati wowote pale ninapoona maandalizi yanalegalega”, amesema Dk Michael Mei 19, 2022 wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika jijini Arusha.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tanzania yaangazi masoko 18 kukuza utalii duniani
- Majaliwa aanika faida za chaneli mpya ya safari Tanzania
Kamati hiyo itakuwa na wenyeviti wenza wawili ambao ni Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Felix John na mwenyekiti mwenza, Rahim Bhaloo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT).
Wenyeviti hao wataongoza kamati ya wajumbe kutoka kwenye baadhi ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, taasisi na idara za wizara mbalimbali, vyama vya wadau wa utalii na waandishi habari wa Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi wa TTB, Felix John amesema, “Mkutano wa 65 wa UNWTO kufanyika Tanzania ni sehemu ya utekelezaji wa vitendo wa mkakati wa Bodi ya Utalii wa kutangaza na kukuza utalii wa mikutano ambao unalenga kuvutia mikutano mingi ya kimataifa kufanyika nchini Tanzania.”
Amewataa wadau wa utalii wajitayarishe kutoa huduma nzuri kwa wageni ili tuendelee kuiweka nchi ya Tanzania kwenye nafasi nzuri ya kuaminiwa kuandaa mikutano mingine ya kimataifa.
Mwenyekiti ZCT, Rahim Bhaloo ameeleza kuwa mkutano huo ni fursa kwa nchi ya Tanzania kuuza mazao ya utalii na uwekezaji katika sekta ya utalii.
Vilevile ni fursa kwa mwananchi kuwa wabunifu ili waweze kufanya biashara na kujiongezea kipatao kupitia mkutano huo.
Latest