Watoa huduma za utalii watakiwa kupata chanjo ya Uviko-19
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro akizungumza na wadau wa utalii pamoja na wataalam mbalimbali walioshiriki katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Umoja wa Ulaya (European Business Group) kwa ajili ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya utalii nchini ambapo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi. Picha| Wizara ya Maliasili na Utalii.
- Waziri Dk Ndumbaro asema wanatakiwa kuwa mfano kwa wengine.
- Itawasaidia kujikinga na kuwakinga wengine.
- Watajenga ujasiri kwa watalii kuingia nchini.
Dar es Salaam. Watoa huduma za watalii nchini Tanzania wametakiwa kuwa mstari wa mbele kupata chanjo ya Corona (Uviko-19), jambo likalosaidia kujikinga na kujenga ujasiri wa watalii kuja kutembelea vivutio vya utalii na wao kufaidika na shughuli hizo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema kama watoa huduma wengi katika sekta ya utalii wachanja itasaidia watalii wanaokuja nchini kupata ujasiri kuwa nchi wanayotembelea ni salama na hivyo hawawezi kupata maambukizi.
“Wanatoa huduma ambao hawajachanjwa wapo hatarini zaidi kupoteza maisha yao kwa vile wanakutana na watu wa kutoka mataifa mbalimbali duniani hususani yale ambayo yana maambukizi makubwa ya Uviko-19. Nawasihi kwa usalama wa maisha yao wachanje” amesisitiza Dk Ndumbaro.
Licha ya kuimarishwa kwa tahadhari katika vituo vya utalii ikiwemo uvaaji barakoa, unawaji mikono, kutumia vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima lakini kwa sasa chanjo ni muhimu zaidi.
“Lazima mtambue kuwa watalii wengi hutokea nchi za Ulaya, Amerika na Asia ambazo hadi wakati huu bado zina viwango vya juu vya maambukizi ya Uviko-19,’ amesema waziri huyo.
Amesema tangu Serikali ya Tanzania iliporidhia kupokea chanjo watalii wameanza kuingia nchini sababu nchi inafuata maelekezo ya watalaam wa afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini ametoa maagizo hayo leo Oktoba 16, 2021 wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Umoja wa Ulaya uliowakutanisha wadau mbalimbali wa utalii nchini kujadili changamoto mbalimbali zinazowikabili sekta ya utalii nchini.
Aidha, wizara anayoiongoza imeshaanza mazungumzo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuona uwezekano wa kuwaruhusu watalii wanaokuja nchini ambao wamepimwa ndani ya saa 72 na waliochanjwa kutokupima tena pindi wanapowasili katika viwanja vya ndege na mipakani.
Amesema hiyo itarahisisha mchakato wa kuvifikia vituo vya utalii katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa sasa, Tanzania inatoa chanjo za aina mbili za Sinopharm ya nchini China na Johnson&Johnson kutoka Marekani.
Latest