Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii

Daniel Mwingira 0528Hrs   Agosti 10, 2018 Safari
  • Bodi ya utalii Tanzania imetangaza maonyesho ya kimataifa ya utalii 22 katika nchi 18.
  • Nchi 10 kati ya 18 yatakapofanyika maonyesho hayo ni masoko makubwa ya utalii Tanzania.
  • TTB itashiriki na kufanya maonyesho mara mbili katika nchi nne katika kipindi cha mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inaangazia kutanua wigo wa kuongeza watalii katika masoko 18 ulimwenguni katika mwaka wa fedha wa 2018/19 baada ya kutangaza rasmi ratiba ya maonyesho 22 ya kimataifa itayoshiriki na kuratibu ikiwa ni fursa kwa kampuni za utalii nchini kusaka watalii zaidi wa nje ya nchi.

Katika taarifa yake iliyotolewa hivi karibuni, TTB imebainisha kuwa maonyesho hayo 22 ambayo itashiriki yatafanyika katika nchi 18 kati ya Julai 2018 na hadi Juni 2019. 

Maonyesho yaliyoangaziwa katika mwaka huu wa fedha ni yale yaliyopo katik nchi za Rwanda, Zimbabwe,  Ufaransa , Kenya, Canada, Uingereza, China, Hispania, Uholanzi na India. Mengine ni ya Marekani, Ubeligiji, Israeli , Afrika Kusini, Ujerumani, Urusi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Korea Kusini.

Uchambuzi zaidi wa Nukta katika ratiba hiyo ya TTB unaonyesha kuwa  bodi hiyo itaratibu na kushiriki maonyesho mengi zaidi barani Ulaya yatakayofanyika katika nchi tisa ikiwa ni idadi kubwa kuliko yale ya mabara ya Amerika Kaskazini, Asia na Afrika. TTB inatarajia kushiriki na kuratibu maonyesho katika nchi nne tu za Afrika zikiwemo mbili za ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki za Burundi na Kenya.

Masoko manne kati ya tisa yanayoangaziwa na TTB mwaka huu ni masoko makubwa ya utalii nchini. Masoko hayo yatainufaisha vilivyo Tanzania ikiwa yatatumika vizuri kutangaza vivutio vilivyopo hasa HIfadhi za Taifa na maeneo ya kihistoria. 

TTB itashiri kwenye maonyesho zaidi ya mara moja katika nchi za China, Ujerumani, Afrika Kusini na Hispania ukilinganisha na maeneo mengine ambayo itashiriki mara moja tu katika kipindi hicho cha mwaka wa fedha.  

Miongoni mwa maonyesho hayo maarufu ni Maonyesho ya Utalii na Uhifadhi ya Kwita Izina ya Rwanda, Maonyesho la Soko la Utalii Ulimwenguni (World Travel Market) yatakayofanyika London, Uiengereza Novemba 2019 na Cape Town, Afrika Kusini mapema Aprili mwakani.

Muonekano wa Mlima Kilimanjaro unaotembelewa zaidi na watalii barani Afrika. Picha| http://entrepreneurs.or.tz

Tanzania inafanya jitihada za kuongeza soko na kuvutia watalii wengi,  wakati ambao mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa unazidi kupaa kila mwaka. 

Kulingana na takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, sekta hiyo inachangia takriban asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP) na zaidi ya robo (asilimia 25) ya mapato yote ya fedha za kigeni. Pia inachangia zaidi ya asilimia 10 ya ajira zote nchini ambapo ajira za moja kwa moja ni 500,000  na ajira takribani millioni moja zisizo za moja kwa moja.

Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Devota Mdachi ameiambia Nukta kuwa wanaendelea kufanya jitihada kubwa katika kutangaza vivutio vya utalii kimataifa kupitia maonyesho mbalimbali ili kuviwezesha kujulikana na kuvutia watalii wengi kuja nchini.

‘’Kwa mara ya kwanza tumeenda kwenye monyesho ya utalii nchini Israeli Januari 2018 katika jitihida hizo hizo za kupanua wigo wa watalii kuja katika vivutio vyetu hapa nchini na mwakani maonyesho hayo yatakuwepo pia,” anasema Mdachi.

Anabainisha kuwa maonyesho hayo ni fursa muhimu kwa kampuni za utalii za ndani na "gharama za ushiriki ni ndogo ambapo kampuni zitakazoshiriki zitawezeshwa na TTB". 

‘’Washiriki huwa wanachangia takribani aslimia 20 ya gharama yote huku asilimia zaidi ya 70 ya gharama ya monyesho hayo zinatolewa na bodi ya utalii kwa kuwa kampuni zote  zitakuwa ndani ya banda la utalii la Tanzania,” anasema Mdachi.

Hatuo hiyo ya TTB, inakuja ikiwa umepita mwezi mmoja tangu Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama na mkewe Michelle Obama kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.

Related Post