Tanzania yachaguliwa makamu wa rais mkutano wa 25 wa UNWTO
- Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki ameiwakilisha Tanzania katika nafasi hiyo.
- Nafasi hiyo inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri katika anga za kimataifa.
Dar es Salaam.Tanzania inaendelea kung’ara katika anga za kimataifa mara baada ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais katika Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) unaofanyika kwa siku tano jijini Samarkand, Uzbekistani.
Kwa mujibu wa kanuni za UNWTO katika kila mkutano ni lazima wajumbe wachague rais na makamu wake ambao huongoza mijadala yote inayofanyika katika mkutano huo.
Kwa mwaka huu nchi ya Tanzania imechaguliwa kushika nafasi ya makamu wa rais ikiwakilishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki aliyeongoza mamia ya wahudhuriaji katika mkutano huo.
Soma zaidi:Idadi ya watalii Tanzania yaongezeka kwa asilimia 25.7
Mkutano huo unaolenga kujadili masuala mbalimbali ya utalii hufanyika kila baada ya miaka miwili na kuhudhuriwa na mawaziri wa utalii wa nchi wanachama wa UNWTO, wadau pamoja na mashirika ya kimataifa yanayoshiriki kama waangalizi.
Akizungumza katika mkutano huo Oktoba 18, 2023 Waziri Kairuki amezishukuru nchi wanachama wa UNWTO kwa kuichagua nchi ya Tanzania katika nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na nchi hizo ili kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii duniani.
Waziri huyo pia amesema kuwa Tanzania itaendelea kuiweka Sekta ya Utalii katika kiini cha maamuzi ya kisiasa na kiuchumi kutokana na mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi, uzalishaji wa ajira na maendeleo mengine.
“Tuungane sote kwa pamoja ili kuiinua zaidi sekta yetu ya utalii kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wetu,” ameongeza Kairuki.
Huenda nafasi hiyo ikaendelea kupaisha shughuli za Utalii zinazofanyika nchini ambazo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inasema zinazidi kuimarika zikichangiwa na kuongezeka kwa wageni wanaotebelea vivutio mbalimbali vilivyopo.
NBS inasema Idadi ya watalii walioingia Tanzania imeongezeka kwa asilimia 25.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
“Hadi kufikia Agosti 2023 watalii 1,131,286 waliingia nchini ulinganisha na watalii 900,182 waliorekodiwa Agosti mwaka jana,” imesema NBS.
Mbali na Tanzania, nchi ya Algeria imeshika nafasi hiyo ya juu katika mkutano huo ikiliwakilisha bara la Afrika huku bara la Amerika likiwakilishwa na nchi za Ajentina na Paraguay.
Bara la Ulaya limewakilishwa na nchi ya Hungary wakati nchi ya Ufilipino imewakilisha Mashariki mwa bara la Asia huku kusini mwa bara hilo kukiwakilishwa na nchi ya Maldives.
Kabla ya Tanzania kushika nafasi ya makamu wa rais wa mkutano wa UNWTO, nchi ya Gambia Ilishika nafasi hiyo mwaka 2021 katika mkutano wa 25 wa Shirika hilo uliofanyika Madrid, nchini Uhispania.