Matumaini mapya sekta ya utalii Tanzania
- Idadi ya watalii wanaoingia nchini yaanza kuongezeka.
- Utalii kuimarika kwa asilimia 60 duniani ifikapo 2022.
- Chanjo ya Uviko-19 kuchangia ongezeko la watalii.
Dar es Salaam. Licha ya sekta ya utalii Tanzania kuathiriwa na janga la Corona, matumaini yameanza kuonekana baada ya idadi ya watalii walioingia nchini mwezi Machi mwaka huu kuongezeka hadi kufikia 71,433.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni kuhusu utalii (High Frequency Data), idadi hiyo imeongezeka kutoka watalii 66,581 waliotembelea vivutio mbalimbali nchini katika kipindi kama hicho mwaka jana sawa na ongezeko la wataliii 4,852.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishi mwezi Machi 2021, sekta ya utalii iliyumba kutokana na athari za janga la Corona (Uviko-19) ikiwemo kuzuia kwa safari za kimataifa.
Licha ya changamoto hizo, idadi ya watalii wanaoingia nchini imekuwa ikipanda na kushuka, jambo linalotoa matumaini kuwa huenda mwaka huu idadi ya watalii ikaongezeka zaidi kwa sababu makali ya Uviko-19 yamepungua.
Mathalan, mwezi Mei mwaka jana ambapo shughuli nyingi za kijamii zilizozuiliwa, Tanzania ilipokea watalii 5,529 tu lakini idadi ilianza kupanda taratibu na kufikia Desemba waliingia watalii 87,605.
Mwezi huo wa Desemba ndiyo kipindi ambacho, Tanzania ilipokea watalii wengi kuliko miezi mingine katika mwaka unaoishi Machi 2021.
Tanzania imejiweka malengo ya kufikisha watalii milioni 5 kwa mwaka ifikapo 2025 na kufanikisha hilo imeongeza wigo wa kutangaza vivutio na kuboresha miundombinu ya utalii ili kuvutia watalii wengi.
Mwaka 2020 pekee Tanzania ilipokea watalii 620,867 ikilinganishwa na watalii milioni 1.5 wa mwaka 2019.

Hali ya utalii duniani
Sekta ya utalii bado ipo katika hali tete duniani kwa mwaka wa pili sasa kutokana na ugonjwa wa Uviko-19,licha ya jitihada mbalimbali za kurejesha sekta hiyo katika hali ya kawaida.
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO), limeeleza kuwaidadi ya wataliiwa kimataifa imepungua kwa asilimia 73 kwa mwaka 2020, huku kwa miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2021, watalii wamepungua hadi milioni 147 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.
Hata hivyo, UNWTO imesema sekta ya utalii duniani itaimarika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022, huku Afrika, sekta hiyo ikitarajiwa kuimarika kwa asilimia 73.
Kampeni ya utoaji chanjo ya Uviko-19 katika mataifa mbalimbali inaweza kuchangia sekta ya utalii kurejea katika hali nzuri, kutokana na kupunguzwa kwa masharti ya safari za kimataifa.
Pia matumizi ya vyeti vya kidijitali vya Uviko-19 (Digital COVID certificate) vitarahisisha safari za watalii maeneo mbalimbali duniani.
Latest
