Tamisemi kutumia Sh7.68 trilioni 2021-22, ikiainisha vipaumbele sita

- Itatumia bajeti ya Sh7.68 trilioni katika mwaka fedha wa 2021/22.
- Bajeti hiyo imeongeza kwa asilimia 8.7 kutoka Sh7.01 trilioni ya mwaka huu.
- Bajeti itajikita zaidi kujenga miundombinu ya elimu na afya.
Dar es Salaam. Ofisi ya Rais Tamisemi inakusudia kutumia Sh7.68 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2021/22 ambapo bajeti hiyo imeongeza kwa asilimia 8.7 ikilinganishwa na iliyotengwa mwaka huu ambapo sehemu kubwa ya bajeti hiyo itaekelezwa katika sekta za afya na elimu.
Katika mwaka wa fedha wa 2020/21, Tamisemi ambayo kwa sasa inaongozwa na Waziri Ummy Mwalimu ilitengewa bajeti ya Sh7.01 trilioni.
“Hadi kufikia Februari 2021, Sh3.9 trilioni zilikuwa zimepokelewa, sawa na asilimia 55.66 ya bajeti (2020/21)yote iliyoidhinishwa,” amesema Waziri Ummy leo Aprili 19, 2021 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake Bungeni jijini Dodoma.
Imesalia siku 73 kumalizika kwa mwaka wa fedha wa 2020/21, jambo linalosubiriwa iwapo Serikali itatekeleza kwa asilimia 100 bajeti hiyo muhimu inayogusa maisha ya watu katika ngazi ya Serikali za mitaa.
Ikiwa Bunge litaidhinisha kiasi cha fedha kilichoombwa na Tamisemi kwa ajili ya mwaka 2021/22 ambao unaanza Julai mosi mwaka huu, bajeti hiyo itakuwa imeongezeka kwa asilimia 8.7 ikilinganishwa na ya mwaka huu ambayo muda wake unaisha Juni 30.
“Naomba Bunge lako likubali na kuidhinisha mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya Sh7.68 trilioni kwa ajili ya Ofisi ya Rais Tamisemi,” amesema Ummy ambaye awali alikuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira wakati wa uongozi wa Rais Hayati John Magufuli.
Kati ya fedha zinazoombwa, Sh4.72 trilioni sawa na asilimia 61.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo yanayojumuisha mishahara ya wafanyakazi wa wizara hiyo.
Aidha, Sh2.95 trilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Sh1.66 trilioni ni fedha za ndani.
Zinazohusiana:
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019/2020
- Dk Mpango-Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
Vipaumbele vya wizara kwa 2021/22
Wakati wa utekelezaji wa bajeti ya Tamisemi mwaka ujao, itazingatia vipaumbele sita ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara za mijini na vijijini, uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuimarisha utawala bora na usimamizi wa rasilimali.
Utoaji wa huduma za afya ya msingi ikijumuisha ununuzi wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa miundombinu ya zahabati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri.
“Utoaji wa elimu ya awali, msingi na sekondari kwa kununua vitabu, vifaa vya maabara pamoja na ujenzi wa miundombinu ya madarasa, maabara, nyumba za walimu, shule pamoja na utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi,” amesema Ummy.
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Tanga Mjini amesema pia watajenga mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji wa viwanda mijini na vijijini.