Tamisemi yaomba kuidhinishiwa Sh11 trilioni mwaka wa fedha 2025-26

April 16, 2025 2:43 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Bajeti yaongezeka kwa Sh Sh1.66 trilioni.
  • Awaagiza wakuu wa mikoa kutekeleza vipaumbele saba ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato.

Dar es Salaam. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeliomba Bunge liidhinishe Sh11.783 trilioni ambazo ni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake.

Fedha hizo zimeongezeka kutoka Sh10.125 trilioni zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambayo Tamisemi iliidhinishiwa hadi kufikia Sh11.783 ikiwa ni ongezeko la Sh1.66 trilioni.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 leo Aprili 16, 2025 bungeni jijini Dodoma, amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha hizo Sh3.95 trilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo 

Baadhi ya Wabunge waliohudhuria katika kikao cha Bunge la kumi na mbili mkutano wa tisa kikao cha saba. Picha/ Ofisi ya Rais Tamisemi.

“Tumewasilisha si tu makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini, ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika. Tamisemi haitafuti sifa ya kisiasa, tunatafuta suluhisho sahihi kwa maisha ya mtanzania wa kawaida,”amesema Mchengerwa.

Hata hivyo, katika jumla ya fedha zilizoobwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo Sh2.5 trilioni ni fedha za ndani ikijumuisha Sh613.44 bilioni za mapato ya ndani ya halmashauri na Sh1.45 trilioni ni fedha za nje.

Mchengerwa amefafanua kuwa Sh7.84 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara Sh6.3 trilioni na matumizi mengineyo Sh1.53 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 66.3 ya bajeti nzima.

Vipaumbele saba vya wizara 

Aidha, Mchengerwa pia amebainisha vipaumbele saba vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwemo kuhakikisha ukusanyaji wa mapato kufikia malengo ambapo amewaagiza wakuu wa mikoa kuwasimamia wakurugenzi wa halmashauri kufanikisha hilo.

Mchengerwa ameongeza kuwa vipaumbele vingine ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, elimu msingi na sekondari kulingana na mipango iliyowekwa, kusimamia utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa uchumi wa kidigitali ikiwemo uwekaji na matumizi ya mifumo na miundombinu ya Tehama katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

 Sambamba na hilo, Mchengerwa ameitaka mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuendelee kuimarisha mifumo stahimilivu na endelevu ya utoaji wa huduma bora za afya, ustawi wa jamii na lishe ili kuboresha huduma ambayo ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote.

“Kuhakikisha mapato katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa yanakusanywa kupitia mifumo ya Tehama ya Serikali pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mifumo hiyo ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato 132…

… Mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha inatekeleza mikakati ya uchumi wa buluu, nishati safi ya kupikia na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira,” amesema Mchengerwa.

Baadhi ya wageni waliohudhuria katika kikao cha Bunge la kumi na mbili mkutano wa tisa kikao cha saba. Picha/ Ofisi ya Rais Tamisemi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks