Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine

Daniel Samson 0833Hrs   Novemba 13, 2018 Habari
  • Amesema uongezaji wa bajeti ya kilimo ni muhimu lakini lazima ufanyike kwa ulinganifu wa mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine za uzalishaji.
  • Mwenendo bora wa kilimo unategemea uwekezaji wa sekta saidizi hasa miundombinu ya umwagiliaji, barabara vijijini, umeme kwa ajili ya kuendesha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.
  • Sekta binafsi yahimizwa kuwekeza katika sekta za kilimo na uvuvi, kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kutafuta masoko ya kikanda na kimataifa.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Isdor Mpango (Mb) amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya kilimo ili kuboresha thamani ya mazao na uzalishaji wa zana za kilimo na uchumi wa viwanda.

Waziri Mpango ametoa kauli hiyo Bungeni wakati akiahirisha mjadala wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2019/2020 na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya  maoni ya wabunge kuhusu kuboresha sekta ya kilimo.

Dk Mpango amesema kuwa uongezaji wa bajeti ya kilimo ni muhimu lakini lazima ufanyike kwa ulinganifu wa mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine za uzalishaji.

“Ni muhimu kukumbuka kuwa sekta ya kilimo ina mwingiliano mkubwa na sekta nyingine. Mwenendo bora wa kilimo unategemea sana uwekezaji wa sekta saidizi hasa miundombinu ya umwagiliaji, barabara vijijini, umeme kwa ajili ya kuendesha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, uzalishaji wa zana za kilimo, dawa, elimu na afya kwa wakulima," amesema Dk Mpango.

Amebainisha kuwa ni muhimu kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika sekta za kilimo na uvuvi, kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kutafuta masoko ya kikanda na kimataifa.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, amewataka wananchi kujishughulisha katika shughuli halali  na kufanya kazi kwa bidii na ufanisi ili kujenga Taifa na kufikia azma ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo inayoajiri watu wengi zaidi nchini.

Kilimo kinaajiri idadi kubwa ya watanzania, uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni muhimu kuboresha maslahi ya wakulima. Picha| travelafricamag.com

Kuhusu kupungua kwa ukwasi katika uchumi hasa fedha katika mifukoni ya wananchi na kwa benki za biashara ambako kumekukuwa kukilalamikiwa na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara, waziri amesema hali hiyo inatokana na kudhibitiwa kwa mianya isiyo halali ya upatikanaji wa fedha, ukwepaji kodi, madai hewa , ufisadi, rushwa, wizi, ubadhilifu wa mali ya umma vimekomeshwa.

Akizungumzia miradi mikubwa inayotajwa kukwama Dk Mpango amefafafanua kuwa miradi iliyokwama imetokana na masharti hasi ya wawekezaji ambayo hayana maslahi kwa Taifa.

“Serikali ina nia ya kuona nchi inaendelea haraka hata hivyo inayo dhamana ya kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinatumika vizuri kwa kulinda maslahi mapana ya Taifa," amesema Mpango

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amesema kuwa Serikali itazingatia maoni na ushauri wa wabunge wote katika Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2019/2020 ili kuhakikisha bajeti ijayo inazingatia vipaumbele vya wananchi. 

 

Related Post