Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019-20
- Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh33.1 trilioni katika mwaka wa fedha ujao wa 2019/20 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.9 kutoka takriban Sh32.5 trilioni ya mwaka huu.
- Utegemezi wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo unatarajiwa kuongezeka kutoka Sh2.68 trilioni mwaka 2018/2019 hadi Sh2.78 trilioni mwaka 2019/2020.
- Serikali yajipanga kuimarisha mapato ya kodi kwa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara na sheria za kodi.
Dar es Salaam. Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh33.1 trilioni katika mwaka wa fedha ujao wa 2019/20 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.9 kutoka takriban Sh32.5 trilioni ya mwaka huu huku utegemezi wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ukiongezeka kidogo.
Utegemezi wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo unatarajiwa kuongezeka kutoka Sh2.68 trilioni mwaka 2018/2019 hadi Sh2.78 trilioni mwaka ujao wa fedha huku Serikali ikiainisha kuwa itaimarisha ukusanyaji wa mapato ya vyanzo ndani ikiwemo ukusanyaji wa kodi.
Katika bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali ilipanga bajeti ya takriban Sh32.5 ambapo makusanyo ya ndani yakijumuisha mapato ya halmashauri yalikuwa Sh20.8 trilioni sawa na asilimia 64 ya makusanyo yote.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20 jijini Dodoma leo (Machi 12,2019), amesema makusanyo ya ndani ambayo yanajumuisha mapato ya halmashauri yatakuwa Sh23 trilioni sawa na asilimia 69.6 ikiwa ni ongezeko la Sh2.15 trilioni ukilinganisha na makusanyo ya mwaka uliopita.
Fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo katika mwaka huo ujao wa fedha zinatarajiwa kuwa Sh12.2 trilioni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ambapo Serikali itaendelea kutekeleza sera za matumizi mazuri ya fedha ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati.
Kiwango hicho cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni kikubwa kidogo ikilinganishwa na asilimia 36 katika mwaka unaoishia Juni 2019.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20 Jijini Dodoma leo (Machi 12,2019). Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Dk Mpango amesema mapato yatokanayo na kodi yanatarajiwa kuwa Sh19.1 trilioni katika mwaka wa fedha ujao kutoka Sh18 trilioni mwaka 2018/19.
Serikali itaimarisha vyanzo vya mapato ya ndani kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya mifumo ya Tehama katika usimamizi wa kodi, Dk Mpango ameeleza.
Soma zaidi: Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
Sambamba na hilo, Serikali imepanga kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na wakala za Serikali na mamlaka za udhibiti.
“Uboreshaji wa mazingira haya utawezesha kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya biashara ambayo kwa ujumla itachangia kuongezeka kwa vyanzo vya mapato,” amesema Dk Mpango katika mkutano huo na wabunge.
“Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya miundombinu na miradi mingine muhimu,” ameongeza Dk Mpango.
Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/2020 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo ni pamoja na viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda; kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu na uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji.