Taasisi za umma zatakakiwa kujiunga vituo vya kidijitali vya TPC

September 6, 2021 1:50 pm · Nuru
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni vituo vya pamoja vya huduma za Serikali.
  • Vinasaidia kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza taasisi za Serikali ambazo hazijaanza kutoa huduma kupitia vituo vya huduma ya pamoja na Shirika la Posta Tanzania (TPC) zihakikishe zinaanza kutoa huduma katika vituo hivyo ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2021/22.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Septemba 6, 2021 wakati akizindua vituo vya huduma pamoja na TPC kwenye viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam na kusema vituo hivyo vitakavyotoa huduma zote za Serikali katika eneo moja kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Baadhi  ya taasisi hizo ambazo bado hazijaanza kutumia huduma hizo ni  Tume ya Ajira, Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania(TMDA), Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

“Uzinduzi wa mradi huu wa huduma za pamoja ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan yenye kuakisi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020. 

“Lengo la Serikali ni kuona mchango wa sekta ya habari na mawasiliano kwenye uchumi unaongezeka sambamba na kutengeneza ajira kwa Watanzania,” amesema Majaliwa.

Aidha taasisi ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kupitia vituo hivyo ni Wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA), UHAMIAJI, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Kwa njia ya Leseni(BRELA),  Shirika la Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma(PSSSF),Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii(NSSF) na Halmashauri za Majiji, hivyo 

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma ambapo kwa sasa huduma hizo zinazotolewa katika vituo vilivyopo kwenye ofisi za Posta za Dar es Salaam na Dodoma.

Pia amesema Serikali itahakikisha miundombinu ya mawasiliano inaboreshwa na wigo wa upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti  kwa gharama nafuu unaongezeka ili wananchi waweze kujiendeleza na kufanya biashara kwa ustawi wa maisha yao.

Kuanzishwa kwa mradi huo ni mageuzi makubwa kwa Shirika la Posta Tanzania ambalo lina ofisi 350 nchini na kwamba hiyo ni hatua muhimu itakayondoa usumbufu na kupunguza gharama kwa wananchi kwani hawatolazimika kutembea maeneo mengi tofauti kufuata huduma moja.

Serikali tayari imetoa Sh3.9 bilioni kwa ajili ya maboresho ya shirika hilo kwenda katika mfumo wa kidijitali.

Awali Kaimu Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo alisema mradi huo wa vituo vya huduma pamoja ni sehemu ya miradi ya Tanzania ya kidijitali ambapo katika mradi huo Serikali imetenga Sh49.5 bilioni. 

Utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika awamu kuu tatu ambapo awamu ya kwanza itahusisha vituo 10 navyo ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya na Morogoro.

Vituo vingine ni Mwanza, Tanga, Kigoma, Mjini Magharibi (Posta Kijangwani) na Kaskazini Pemba (Chake Chake).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW