Majaliwa: Teknolojia itasaidia kukabiliana na rushwa,ubadhirifu nchini
- Asema ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwa kasi.
- Waziri Nape ataja nguzo tano zinazoongoza mapinduzi ya Tehama nchini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, amebainisha kuwa Serikali inapigia chapuo maendeleo ya sayansi na teknolojia katika utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo za kijamii nchini ili kukabiliana na rushwa pamoja na ubadhirifu.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la wadau wa teknolojia la ‘Future Ready Summit’ (FRS) leo Februari 15, 2024 amewaambia washiriki kuwa maendeleo ya teknolojia katika utoaji huduma yatapunguza muda pamoja na watu kuonana ana kwa ana jambo litakalosaidia kuziba mianya ya rushwa.
“Serikali chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kuimarisha kuhakikisha kila huduma hapa nchini inatolewa kidijitali…
…na kwa kufanya hivyo tutapunguza rushwa, ubadhirifu, wizi, ili kila mmoja atumie alichonacho kupata huduma anayoitaka kwa gharama ile ile, hatua hii ndiyo ambayo sisi tunaendelea nayo kwa kasi,” amesema Majaliwa.
Soma zaidi:Teknolojia ya kuteketeza taulo za kike (pedi) itakavyookoa mazingira Tanzania
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu, inakuja wakati ambao tayari wadau wa maendeleo wamekuwa wakiishauri Serikali kuboresha mifumo ya utoaji huduma kuwa ya kidijiti ili kurahisisha upatikanaji wake kwa kuepusha milolongo mirefu isiyo na lazima.
Miongoni mwa huduma zinazofanyika kidijiti hivi sasa ni pamoja na maombi ya hati ya kusafiria ‘Passport’, pamoja na maombi ya Namba ya Mlipa Kodi (TIN).
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ili kufanikisha upatikanaji wa huduma za kidijiti Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo minara mipya pamoja na kuipandisha hadhi minara kwenda katika teknolojia ya 2G, 3G na 4G.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kulia) akisikiliza jambo wakati akitembelea mabanda ya maonyeshokatika kongamano la ‘Future Ready Summit’ jijini Dar es Salaam.Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu/Twitter.
Kwa upande wake Waziri wa Habari Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Nape Nnauye, amesema Serikali inandelea kutengeneza msingi imara wa kisheria utakaosaidia upatikanaji, uendelezaji na uanzishaji wa huduma za teknolojia.
“Pale wizarani tumekubaliana na wenzangu tuwe na misingi mitano inayotuongoza, ambayo ni upatikanaji wa huduma, unafuu, ubora, usalama pamoja na matokeo chanya,” amesema Waziri Nape.
Kongamano la FRS limewakutanisha wadau katika sekta ya teknolojia ikiwemo wawekezaji, watunga sera, na wabunifu wa teknolojia kujadili changamoto, fursa pamoja na mikakati ya kuendeleza matumizi ya teknolojia kujiletea maendeleo.