Sarafu 5 zenye nguvu zaidi duniani
- Ukiwa na kiasi kidogo cha sarafu hizo unaweza kupata Dola nyingi zaidi.
Dar es Salaam. Watu wengi hudhani kuwa Dola ya Marekani ndiyo sarafu yenye nguvu zaidi duniani kwa sababu ndiyo hutumika sana katika biashara za kimataifa, mikataba ya mafuta au hata akiba za mataifa mengi.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba Dola ya Marekani si sarafu yenye thamani kubwa zaidi inapolinganishwa na sarafu nyingine duniani. Kuna sarafu kadhaa ambazo zina nguvu zaidi kuliko Dola ya Marekani,
Hii ina maanisha kuwa ukiwa na kiasi kidogo cha sarafu hizo unaweza kupata Dola nyingi zaidi.
Sarafu ya tano ni Pauni ya Uingereza, hii ni moja ya sarafu kongwe na imara duniani.Wakati Dola moja ya Marekani ni takriban Sh2,600, Pauni moja ya ni zaidi ya Sh3,000 na ni takriban Dola 1.25 ya Marekani.
Nafasi ya nne inashikiliwa na Dinar ya Jordan. Hii ni sarafu ya nchi ambayo si kubwa sana kiuchumi, lakini ina thamani kubwa sana. Dinar 1 ya Jordan ni sawa na takribani Dola 1.41 za Marekani, au zaidi ya Sh 3,600 za Tanzania.
Katika nafasi ya tatu ipo Rial ya Oman. Hii ni sarafu yenye nguvu sana kutokana na uchumi wa mafuta wa nchi hiyo. Rial 1 ya Oman ni sawa na takribani Dola 2.60 za Marekani, au zaidi ya Sh6,700 za Tanzania. Hii ina maana kuwa Dola moja ya Marekani ni ndogo sana ikilinganishwa na Rial ya Oman.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Dinar ya Bahrain. Hii pia ni sarafu yenye nguvu kubwa sana duniani. Dinar 1 ya Bahrain ni sawa na takribani Dola 2.65 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh6,800 za Tanzania.
Hatimaye, nafasi ya kwanza inashikiliwa na Dinar ya Kuwait, ambayo ndiyo sarafu yenye nguvu zaidi duniani kwa sasa. Dinar 1 ya Kuwait ni sawa na takribani Dola 3.25 za Marekani, au zaidi ya Sh8,000 za Tanzania. Hii inamaanisha kuwa Dola moja ya Marekani haifikii hata robo tatu ya nguvu ya Dinar ya Kuwait.
Sababu ni nini ?
Hata hivyo kuna sabu kadhaa zinazofanya sarafu ya taifa fulani kuwa na thamani zaidi ya sarafu za mataifa mengine.
Moja kati ya mambo yanayofanya sarafu hizi kuwa na thamani zaidi ni nguvu ya uchumi wa nchi husika, hasa mapato ya nje. Kwa mfano, Kuwait, Oman na Bahrain zinapata mapato makubwa sana kupitia mauzo ya mafuta kwenye soko la dunia.
Kwa kuwa mafuta yanauzwa kwa Dola za Marekani, nchi hizi huingiza kiasi kikubwa cha fedha za kigeni ukilinganisha na matumizi yao ya ndani, jambo linalofanya sarafu zao kuwa na nguvu zaidi.
Sababu nyingine muhimu ni sera ya kifedha na namna serikali inavyodhibiti sarafu yake. Nchi kama Kuwait haziruhusu sarafu zao kuogelea kwa uhuru kwenye soko la dunia kama ilivyo kwa Dola ya Marekani au Euro. Hii husaidia kuzuia kushuka kwa thamani na kuifanya sarafu kuwa imara zaidi.
Pia, uwepo wa akiba kubwa ya fedha za taifa (sovereign wealth funds) huchangia sana. Nchi hizi huwekeza mapato ya mafuta kwenye miradi na masoko ya kimataifa, hivyo kuongeza uthabiti wa uchumi wao kwa muda mrefu. Hii hujenga imani ya wawekezaji na taasisi za kifedha duniani, na hatimaye kuipa sarafu nguvu zaidi.
Sababu nyingine ni idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na mapato ya taifa. Nchi kama Kuwait zina watu wachache lakini mapato makubwa sana ya mafuta.
Hii ina maana kila mtu ananufaika na pato kubwa la taifa, jambo linaloongeza nguvu ya ununuzi wa ndani na kuimarisha thamani ya sarafu.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo anasema kwa jicho la kiuchumi si tatizo kuwa na sarafu yenye thamani zaidi kuliko dola, bali kuwa na sarafu inayobadilika badilika thamani kila wakati kwani kuna mataifa makubwa ambayo yana sarafu dhaifu kuliko dola lakini yana uchumi imara.