Ukame wasababisha mifugo zaidi ya 1,200 kufariki Kilimanjaro
- Kutonyesha kwa mvua za vuli kwasababisha ukosefu wa malisho na maji.
- Mifugo 1,257 wakiwemo ng’ombe 841 yafariki.
- Mkoa wasema unajitosheleza kwa chakula.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai amesema mifugo 1,257 zikiwemo ng’ombe 841 imeripotiwa kufa katika mkoa huo kwa kukosa malisho na maji kutokana na ukame unaoendelea katika baadhi ya maeneo ikiwemo Wilaya ya Mwanga.
Kigaigai aliyekuwa akizungumza leo Januari 22, 2021 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan katika tamasha la utamaduni mkoani Kilimanjaro amesema kwa sasa ukame uliosabishwa na kutonyesha kwa mvua za vuli ndiyo changamoto kubwa kwa wakazi wa mkoa huo.
Ukame huo umeleta madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya mifugo 1,257 vilivyotokana na kukosa maji na malisho.
“Changamoto kubwa inayotukabili sisi wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa ni kutonyesha kwa mvua za vuli hali iliyosababisha ukame na ukosefu wa malisho ya mifugo katika baadhi ya maeneo hususani Wilaya za Mwanga na Same ambapo jumla ya ng’ombe 841, kondoo 406, punda 10 wameripotiwa kufa hadi sasa kwa kukosa malisho na maji,” amesema Kigaigai.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo, mkuu wa mkoa huyo amemuhakikishia Rais Samia kuwa mkoa umejitosheleza kwa chakula.
“Hii ni kutokana na kuwa na ziada ya uzalishaji wa chakula tano 47, 790 za wanga na tano 10,147 za mikunde katika msimu wa mvua za mwaka 2020/21,” amesema Kigaigai na kuongeza kuwa,
“Bado tuna uhakika wa wananchi kupata chakula katika mwaka huu unaoendelea.”
Msimu wa mvua za vuli ambao huanza Oktoba na kuisha Desemba ni mahsusi kwa maeneo ya mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwemo Arusha, Manyara, Kilimanjaro, kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Mafia.
Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
TMA katika taarifa iliyotolewa Septemba 2, 2021 ilisema kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua hizo, jambo linaweza kusababisha ukame.
Mbali na mvua za chini ya wastani hadi wastani, vipindi vya joto kali kuliko kawaida vimetokea katika msimu wa vuli.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Ujio mvua za vuli: Wakulima, wavuvi watahadharishwa Tanzania
- Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania – 1
Rais Samia aingilia kati
Kutokana na athari walizopata wafugaji wa mkoa huo wa kupoteza mifugo yao, Rais Samia amewapa pole hukua akibainisha kuwa mvua za vuli zimeanza kunyesha na zitatua changamoto ya malisho na majik
“Hili ni janga kubwa na naomba nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi wa Kilimanjaro na mikoa mingine ambayo tumekumbwa na maafa mbalimbali hususan mikoa ya Manyara na Arusha kwamba athari za janga hili zimekuwa kubwa kuliko maeneo mengine,” amesema na kuongeza kuwa,
“Tunatarajia mvua zilizoanza kunyesha hivi sasa zitaendelea ili zitutoe katika maafa ya ukame uliotukumba.”Aidha, Rais Samia amewataka wafugaji kushirikiana na Serikali kutumia mafunzo waliyopata katika janga hilo kuona namna bora ya kuanza ufugaji wa kisasa usiotegemea mvua katika kupata malisho.
“Kwa upande wetu Serikali tumejiandaa vyema tutakuja kwenu kuonyesha jinsi ya kupata malisho bila ya kutegemea mvua kuepuka athari hizi zinazoletwa na ukame,” amesema Rais Samia.