Vodacom, Tafina zitakavyoshiriki kongamano la uwekezaji Afrika Mashariki

March 13, 2026 3:32 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Kongamano hilo litafanyika Machi 26 na 27, 2026 jijini Dar es Salaam.
  • Litawaleta pamoja viongozi kutoka sekta za fedha, teknolojia, udhibiti, na uwekezaji ili kuendeleza uchumi wa kidijitali wa ukanda huu.

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya simu Vodacom Tanzania itakua mdhamini mkuu wa Kongamano la Uwekezaji Afrika Mashariki (EAIF 2026) litakalojadili namna ya kuendeleza uchumi wa kidijitali wa ukanda huo.

EAIF inayoratibiwa na Chama cha Watoa Huduma za kifedha kwa Kutumia Teknolojia (Tafina) kwa mwaka huu itafanyika jijini Dar es Salaam, Machi 26 na 27 mwaka huu.

Kongamano hilo litawaleta pamoja viongozi kutoka sekta za fedha, teknolojia, udhibiti na uwekezaji ikiwemo Vodacom Tanzania kupitia huduma yake ya kifedha mtandaoni ya M-Pesa. 

Katibu Mkuu wa Tafina, Shadrack Kamenya aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam amesema kuwa ushirikiano wa Vodacom katika kongamano hilo unaonyesha imani ya sekta binafsi katika ukuaji wa chama hicho nchini Tanzania.

“Ushirikiano wa Vodacom katika EAIF 2026 unaonyesha uongozi na imani katika sekta ya ‘fintech’ ya Tanzania na uchumi mpana wa kidijitali. Hii ni hatua muhimu katika kujenga miundombinu ya ubunifu, kusaidia wajasiriamali na kuifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu cha uwekezaji wa fintech,” amesema Kamenya.

Meneja wa Sera na Uhusiano wa Jamii wa Vodacom Tanzania, Buberwa Mukurasi, akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Picha| Wingod Odemary.

Tafina ni umoja wa watoa huduma za kifedha kupitia teknolojia nchini Tanzania unaolenga kukuza mfumo wa kifedha ulio hai, jumuishi, na bunifu kupitia utetezi wa sera, ushirikiano wa wadau na uimarishaji wa uwezo wa sekta.

Meneja wa Sera na Uhusiano wa Jamii wa Vodacom Tanzania, Buberwa Mukurasi, amesema kampuni hiyo inajivunia kushirikiana na Tafina kama mdhamini wa kongamano hilo linalofanyika kwa awamu ya pili toka kuanzishwa kwake mwaka 2024.

Amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya dhati ya Vodacom katika kuendeleza ujumuishaji wa huduma za kifedha kwa njia za kidijitali na kuchochea uwekezaji katika sekta ya fintech katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kwa miaka mingi, huduma ya M-Pesa imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ujumuishaji wa kidijitali na kifedha, tukiongozwa na dhamira yetu ya kuwaunganisha watu kwa ajili ya kuboresha maisha yao,” amesema Mukurasi.

Kwa mujibu wa Ripoti za Takwimu za Robo ya Mwaka 2025 zinatolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Septemba 2025 Vodacom ilikuwa inamiliki asilimia 31.5 ya soko la mawasiliano ya simu Tanzania.

Meneja wa Mahusiano wa Tafina Juliet Kiluwa, amesema kuwa kongamano hilo litajumuisha mijadala ya kitaalamu, mikutano ya kuunganisha wadau wa biashara, majadiliano ya kimkakati kuhusu ukuaji wa sekta ya Tafina na kuunganisha miradi ya maendeleo na fursa za ufadhili kupitia teknolojia, ubunifu na ushirikiano wa kisekta.

Hadi sasa, Tafina ina wanachama zaidi ya 80 wanaounda jumuiya ya watoa huduma za kifedha kupitia teknolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks