Mvua za vuli kuleta maumivu Tanzania

Daniel Samson 1012Hrs   Septemba 02, 2021 Habari
  • Mvua zisizoridhisha zinatarajiwa kuathiri uzalishaji wa mazao, umeme na madini huku sekta ya usafirishaji ikineemeka.
  • Kuna uwekezano wa kutokea ukame.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za vuli katika kipindi cha Oktoba mpaka Desemba mwaka huu hazitarajiwi  kuwa za kuridhisha katika baadhi ya maeneo ya nchi hivyo kuathiri sekta mbalimbali zikiwemo nishati na kilimo. 

TMA imesema kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua hizo, jambo linaweza kusababisha ukame.

Mbali na mvua za chini ya wastani hadi wastani zinazotarajiwa, vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa vuli.

Msimu wa mvua za vuli ni mahsusi kwa maeneo ya mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka  ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Mafia.

Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Athari zinazotarajiwa

TMA katika taarifa iliyotolewa leo Septemba 2, 2021 imeeleza kuwa kutokana na kusuasua kwa mvua hizo sekta mbalimbali zinaweza kuathirika iwapo wahusika hawatachukua tahadhari kukabiliana nazo.

Miongoni mwa sekta zitakazoguswa na athari hizo ni kilimo ambapo upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za vuli hasa nyanda za juu kaskazini na ukanda wa pwani ya kaskazini ambapo hali hii inaweza kuathiri ukuaji wa mazao. 

“Ongezeko la visumbufu vya mazao kama mchwa, viwavi jeshi, panya na magonjwa vinatarajiwa kujitokeza katika msimu na hivyo kuathiri mazao na uzalishaji kwa ujumla,” imeeleza TMA katika taarifa yake.

Wakulima wanashauriwa kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa ndani ya muda mfupi na yanayostahimili ukame na kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji.

Athari hizo pia zitaiguza sekta ya mifugo na uvuvi ambapo upungufu wa mvua katika msimu unatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na upatikanaji wa chakula kwa ajili ya samaki. 

“Baadhi ya magonjwa ya mifugo (yanayoenezwa na kupe pamoja na wadudu warukao) na samaki yanatarajiwa kupungua, lakini vifo vya wanyama kutokana na ukame na magonjwa nyemelezi yanatarajiwa kuongezeka,” imeeleza taarifa hiyo kuwa kuna uwezekano wa migogoro kujitokeza baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Upungufu wa mvua katika msimu wa vuli unaweza kuathiri uzalishaji wa samaki, umeme na kilimo. Picha| Gift Mijoe.

Nishati, maji na madini vinaweza kuathiriwa

Upungufu wa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini unatarajiwa kujitokeza na hivyo kuathiri uzalishaji wa madini (hususan dhahabu kwa wachimbaji wadogo) na nishati ya umeme utokanao na maji.

Hata hivyo, TMA imesema utekelezaji wa miradi ya umeme, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi unatarajiwa kuendelea vizuri huku wadau wakisisitizwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji katika shughuli hizo. 

Pia upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama unaweza kujitokeza na kusababisha mlipuko wa magonjwa ambapo mamlaka za afya zinashauriwa kuchukua hatua stahiki kupunguza athari hasi, ikiwa ni pamoja na kuhimiza wananchi kutibu maji kabla ya kutumia, kunywa maji safi, salama, na ya kutosha ili kuepuka upungufu wa maji mwilini.

Licha ya maeneo mengi kukosa mvua, kuna uwezekano wa kutokea kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa ambavyo vinaweza kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu. Picha| Gift Mijoe.


Neema kwa wengine

TMA imesema maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, hivyo sekta ya usafiri na usafirishaji hususan usafiri wa ardhini inaweza kunufaika kutokana na vipindi vya ukavu vinavyoweza kujitokeza. 

“Hata hivyo, inashauriwa kuwa mipango ya uboreshaji wa miundombinu ifanyike kwa kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa katika eneo husika,” imesisitiza taarifa hiyo.

Licha ya maeneo mengi kukosa mvua, kuna uwezekano wa kutokea kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa ambavyo vinaweza kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

Related Post