Mapendekezo ya tume kudhibiti matumizi mseto ya ardhi Ngorongoro

March 12, 2026 4:49 pm · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaitaka Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro.
  • Mamlaka yatakiwa kuwapa cheti maalum wakazi wa Ngorongoro.

Arusha/Dar es Salaam. Tume ya Rais ya kutathmini kuhusu masuala ya mgogoro wa ardhi ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imetoa mapendekezo ya taratibu na sheria zitakazodhibiti matumizi mseto ya ardhi katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa tume hiyo Dk Gerald Ndika aliyekuwa akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan leo Machi 12, 2026, ikulu Chamwino mkoani Dodoma amesema ili kudhibiti matumizi ya ardhi hiyo ni lazima Serikali ifanye maboresho ya Sheria ya Ngorongoro namba 284.

“Tume inapendekezwa kuwa Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro namba 284 ifanyiwe mapitio na marekebisho kwa kuwashirikisha wadau wote muhimu ili iendane na wakati na mahitaji ya sasa,” amesema Dk Gerald.

Ripoti hiyo ya tume iliyoundwa na Rais Samia Desemba, 2024 ni miongoni mwa masuala yaliyosubiriwa sana na Wananchi pamoja na wadau wa masuala ya haki za binadamu baada ya kutokea kwa sakata la wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro kupinga kuondolewa katika eneo hilo.

Licha ya Serikali kutenga maeneo mengine kwa ajili ya kuwahamishia wakazi hao ikiwemo Msomera jijini Tanga, suala hilo lilizua mgogoro uliopelekea Rais Samia kuunda tume hiyo pamoja na nyingine iliyolenga kutathmini zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi hao.

Mapendekezo mengine yaliyowasilishwa na tume hiyo ni wananchi  kuruhusiwa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi nje ya eneo la hifadhi na wakazi hao kupewa vyeti  maalum vya utambulisho.

“Ili kuondoa uvamizi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro mamlaka iwatambue na kuwaorodhesha kwenye kanzi data wakazi wote wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro, makazi yao mifugo na kuwapa cheti kulingana na matakwa ya kifungu cha 284 cha Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro,” amesema Gerald.

Aidha, tume hiyo imebainisha kuwa zoezi la uhamaji katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro liweendelevu likiambatana na ukarabati wa miundombinu.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa akizungumza leo amewahakikishia wananchi wa Ngorongoro kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika hatua zote za utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na tume hizo akisisitiza kuzitunza hifadhi hizo.

“Niwaombe Watanzania wenzangu kulipa kipaumbele swala la uendelevu wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine ya hifadhi. Ngorongoro ni almasi yetu Tanzania, ni mali yetu Tanzania lakini pia ni urithi wa dunia,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.Picha|Ikulu Mawasiliano.

Wachambuzi watia neno

Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof Omari Mbura ameiambia Nukta Habari kuwa uamuzi kutenganisha matumizi ya ardhi kutasaidia kupunguza mgongano wa shughuli na kuondoa usumbufu unaoweza kutokea kutokana na mwingiliano wa moja kwa moja.

Kwa mujibu wake pendekezo hilo linaweza kuwa na tija kwa Serikali, likiwasaidia kulinda wanyamapori ambao pia ni chanzo cha mapato kupitia utalii huku ikiwapunguzia wananchi migogoro kati yao na wanyama.

Naye Paul Chengula, mchumi kutoka Dar es Salaam anasema kuwa endapo wananchi wataruhusiwa kufanya shughuli za kiuchumi kama kilimo, itawasiaida kuboresha maisha yao na kuingiza kipato cha ziada.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks