Maswali magumu mikoa 10 maskini zaidi Tanzania

Nuzulack Dausen 0651Hrs   Januari 21, 2020 Chati & Data
  • Rukwa ndiyo unaoongoza kwa kuwa na takriban nusu au asilimia 45 ya watu wake ambao hawawezi kumudu mahitaji ya msingi wakati Dar es Salaam ukiwa na watu wachache wasiokuwa na uwezo huo kwa asilimia nane tu

Dar es Salaam. Licha ya kiwango cha umaskini Tanzania kupungua ndani miaka 10 iliyopita nchini Tanzania, bado kuna mikoa inayokabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini wa mahitaji ya msingi ambacho kimewekwa kuwa ni takriban Sh50, 000 kwa mwezi. 

Ripoti ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katikati ya mwaka jana inabainisha kuwa kiwango cha Watanzania wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi nchini kimepungua hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18 kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12.

“Umaskini wa mahitaji ya msingi ulishuka karibu kila maeneo kwa kasi katika maeneo ya vijijini. Ndani ya muongo uliopita, uwiano wa Watanzania ambao wapo katika umaskini wa kutopea na ambao hawawezi kumudu kununua chakula kinachoweza kutimiliza viwango vya kilokalori (Kcal) 2,200 kwa siku ulishuka kutoka asilimia 12 hadi asilimia nane,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Hata hivyo, kuna mikoa ambayo zaidi ya theluthi ya watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi ambao ni Sh49,320 kwa mwezi kwa mtu mzima kwa mujibu wa utafiti huo wa mwaka 2018. 

Baadhi ya mikoa hiyo ni Rukwa, Simiyu, Lindi, Geita, Mwanza, Tabora, Kigoma, Tabora na Singida. 

Rukwa ndiyo unaoongoza kwa kuwa na takriban nusu au asilimia 45 ya watu wake ambao hawawezi kumudu mahitaji ya msingi wakati Dar es Salaam ukiwa na watu wachache wasiokuwa na uwezo huo kwa asilimia nane tu. 

Takwimu hizo zinaibua maswali lukuki juu ya hali katika mikoa 10 inayoongoza kwa kuwa na viwango vikubwa vya umaskini wa mahitaji ya msingi. Miongoni mwa maswali hayo ni kwanini kuna viwango vikubwa vya umaskini katika mikoa hiyo? Ni mikakati gani inaweza kuikwamua na hali hiyo? 

Related Post