Kipindupindu kina chanjo?

Mwandishi Wetu 0813Hrs   Aprili 13, 2023 NuktaFakti
  • Ndiyo, ugonjwa huo wa mlipuko una chanjo za aina tatu kwa sasa.
  • Upatikanaji wa maji na salama, vifaa vya kujisafi na usafi ni muhimu. 

Dar es Salaam.  Ugonjwa wa kipindupindu umeripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani hasa katika nchi za Afrika. 

Kutokana na ugonjwa huo wa kuambukiza kuathiri maisha ya watu ikiwemo kugharimu maisha, baadhi ya watu wenye nia mbaya wamekuwa wakisambaza uzushi/uongo ili kuzidisha madhara.

Moja ya uzushi huo ambao unaenezwa mtandaoni ni kuwa ugonjwa huo hauna chanjo huku wengine wakiamini kuwa chanjo zilizopo hazina ufanisi kumkinga mtu kama ilivyo kwa Uviko-19. 

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limekanusha madai hayo na kueleza kuwa kuna chanjo aina tatu zinazoweza kumkinga mtu na kipindupindu ikiwemo ya ‘Shanchol’ na Euvichol-Plus.

Kwa sasa, dozi moja ya chanjo inatolewa kwa njia ya kinywa na siyo mbili kwa sababu ya uhaba wa afua hiyo dhidi ya kipindupindu duniani.

Chanjo ni salama na ina ufanisi mkubwa uliothibitishwa na watalaam wa afya kukinga dhidi ya ugonjwa huo ambao umelipuka katika maeneo mbalimbali duniani kwa sasa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko. 

WHO inaeleza kuwa chanjo hiyo inaweza kutolewa kwa watoto kuanzia miaka sita na watu wazima wakiwemo wajawazito.

Unaweza kupata chanjo hiyo kwa njia ya kumeza lakini upatikanaji maji safi na salama, miundombinu ya kujisafi na usafi ni mambo muhimu ya kuzingatia kumlinda mtu na ugonjwa huo.


Kipindupindu nini?

Kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya ‘vibrio cholera’ kwenye utumbo mwembamba, ambaye hutoa sumu inayosababisha kutolewa kwa maji mengi ndani ya utumbo, kwa njia ya kuhara, wakati mwingine kutapika na homa kali.

Bakteria huyu anapatikana katika chakula au maji machafu na kinyesi kutoka mtu aliye na maambukizi. Kwa ujumla unaweza kuambukizwa kupitia maji machafu, mboga zilizopandwa kwenye maji taka¸ samaki na dagaa waliovuliwa kwenye maji machafu, vyakula na vinywaji vilivyo na bakteria huyu kutokana na uchafu

Dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni chache na ni rahisi kwa mtu kuweza kuzibaini na zinaweza kuonekana ndani ya saa hache au siku tano baada ya maumbukizi. Dalili hizo ni:

  • Kuharisha maji maji yanayofanana na maji ya mchele
  • Kutapika
  • Kujisikia mlegevu, kukosa nguvu
  • Wakati mwingine kusikia maumivu ya misuli
  • Upungufu wa maji mwilini
  • Kuna wakati mgonjwa anakuwa na ngozi iliosinyaa na mdomo kukauka


Related Post