Mkaa, samani vyachangia kupandisha mfumuko wa bei Tanzania

Esau Ng'umbi 1026Hrs   Mei 08, 2024 Biashara
  • Waongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3 iliyokuwepo Machi.
  • Ni kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za chakula.
  • Hili ni ongezeko kubwa la kwanza kurekodiwa baada ya miezi minne.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini kwa mwaka unaoishia Aprili 2024 imeongezeka kiduchu hadi asilimia 3.1 ukichangiwa zaidi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za vyakula.

Ongezeko hilo ni la kwanza kurekodiwa ndani ya kipindi cha miezi minne iliyopita ambapo kiwango kikubwa zaidi kilirekodiwa mwaka ulioishia Novemba 2023 cha asilimia 3.3.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Mei 8, 2024 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024 umeongezeka kidogo hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi 2024.

Mkaa wachangia kupandisha mfumuko wa bei

NBS imeeleza kuwa ongezeko hilo limechangiwa zaidi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo vyakula ukiwemo mkaa uliongezeka kutoka asilimia 15.7 hadi 21.5 na samani za nyumbani kutoka asilimia 4.5 hadi 4.8). 

“Mfumuko wa bei wa magodoro umeongezeka kutoka asilimia 3.5 hadi 5.1, huduma ya malazi kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni (kutoka asilimia 2.6 hadi 3.8), petroli (bei imeongezeka kwa asilimia 2.1) na mafuta ya taa bei imeongezeka kwa asilimia hadi 2.0,” imebainisha taarifa hiyo ya NBS.

Tofauti na bidhaa zisizo za vyakula, taarifa ya NBS imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024 umebaki katika asilimia 1.4 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2024.


Soma zaidi: Haitakuwa rahisi kufikia lengo la asilimia 80 nishati safi ya kupikia - Rais Samia


Hata hivyo, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024 umeongezeka hadi asilimia 3.9 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2024 huku.

Kwa mujibu wa NBS mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula visivyochakatwa umebaki katika asilimia 3.9 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2024 ukichangiwa zaidi na misukosuko ya uchumi inayoendelea duniani ikiwemo vita ya Urusi na Ukraine pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Mapema Aprili Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliongeza riba ya benki kuu hadi asilimia 6 kutoka asilimia 5.5 ili kudhibiti mfumuko wa bei hasa unaochochewa na visababishi vinavyoendelea katika soko la dunia. 

Tanzania kinara EAC

Licha ya mfumuko wa bei kuongezeka kiduchu, Tanzania bado imeendelea kuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Madhariki ambapo Kenya ina asilimia 5 na Uganda asilimia 3.2 kwa Mwaka ulioishia Mwezi Aprili.

Related Post