Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania

Daniel Mwingira 0213Hrs   Agosti 11, 2018 Safari
  • Milima tisa kati ya 10 mirefu zaidi Tanzania inapatikana katika mikoa mitatu tu ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
  • Mlima Kilimanjaro ndiyo mlima mrefu zaidi nchini na barani Afrika.
  • Mlima Rungwe ambao huaminika kuwa kilele cha Nyanda za Juu Kusini umepitwa kwa mita moja na Mlima Mtorwi hivyo kuondolewa kwenye orodha ya milima 10 mirefu zaidi.

Dar es salaam. Iwapo utapewa swali utaje milima 10 mirefu zaidi Tanzania huenda usijibu swali hilo kirahisi? Haupo pekee yako. Wengi wanaijua zaidi Mlima Kilimanjaro kutokana na upekee wake katika bara la Afrika. Ni wachache sana wanaoweza kutaja au kuielezea kwa ukamilifu milima mengine mirefu nchini ambayo nayo ina vivutio lukuki vya utalii.

Ripoti ya Utafiti ya Wageni wa Kimataifa ya mwaka 2016 (The 2016 International Visitor Exit Survey Report) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Oktoba mwaka jana inaeleza kuwa upandaji wa milima ni kuvutio cha tatu kwa wageni wa nje wanaoingia nchini kwa mara ya kwanza baada ya utalii wa wanyamapori na ufukweni.

Kama bado unasaka majina ya milima hiyo 10 usiwaze. Nukta inakuletea orodha ya  milima 10 mirefu Tanzania, mikoa ilipo, urefu na fursa za kitalii zinazoweza kupatikana katika rasimali hizo.

Uchambuzi zaidi za takwimu muhimu za mwaka 2016 za NBS (Tanzania in figures 2016) unabainisha kuwa milima  tisa kati ya 10 mirefu zaidi nchini ipo katika mikoa miwili tu ya Kilimanjaro na Arusha. Ni mlima mmoja uitwao Mtorwi ndiyo unapatikana mkoani Iringa. 

Ifuatayo ni orodha ya milima 10 mirefu zaidi Tanzania: - 


Mlima Kilimanjaro, 5,895 (Kilimanjaro)

Mlima Kilimanjaro siyo tu ni mlima zaidi nchini bali katika bara zima la Afrika. Mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,340) pia ni hifadhi ya Taifa. Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 755 na iko umbali wa kilometa 45 kutoka Moshi mjini. Kilele cha Kibo ndio kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na kufunikwa na theluji.

Mlima huo unaopatikana katika mkoa wa Kilimanjaro ni moja kati ya milima ambayo kilele chake hufikiwa kwa urahisi na hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wapanda milima kutoka kila pande za dunia.

Mlima Kilimanjaro ukionekana kwa mbali. Kilimanjaro ndiyo mlima mrefu zaidi nchini na barani Afrika. Picha| Mtandao.


Mlima Meru, mita 4,566 (Arusha)

Mlima wa pili kwa ukubwa Tanzania ni Mlima Meru wenye kilomita za mraba 4,566 (futi 15064) kutoka usawa wa bahari ikiwa ni tofauti ya mita 1329 kutoka Mlima Kilimanjaro. Katika anga za kimataifa, Mlima Meru unashika nafasi ya tisa kwa urefu barani Afrika .

Mlima Meru unapatikana ndani ya Hifadhi ya Arusha ambayo ilianzishwa mwaka 1960. Baadhi ya wa wanyamapori waliopo katika hifadhi waliletwa kutoka katika maeneo mengine na hupenda kuzungukazunguka katika Mto Momella na Kreta ya Ngurudoto (Ngurudoto crater). Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 137 na ipo umbali wa kilometa 35 kutoka mji wa kitalii wa Arusha na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Inaelezupanda Mlima Meru kunachukua siku tatu hadi nne na wakati mzuri kwa kupanda mlima ni kuanzia mwezi Juni hadi Februari ambapo mvua zinaweza kunyesha katika mwezi Novemba. Na wakati mzuri wa kuona mlima Kilimanjaro kutokea Meru ni kati ya Desemba na Februari.


Mlima Klute, mita 3,952 (Kilimanjaro)

Mlima Klute ni mlima unaoshika nafasi ya tatu kwa ukubwa hapa Tanzania. Mlima huo wenye urefu wa mita 3,952  unapatikana katika mkoa wa Kilimanajaro ikiwa ni tofauti ya mita zipatazo 1,943 na Mlima Kilimanjaro.


Mlima Lool Malasin, 3,626 (Kilimanjaro)

Mlima Lool Malasin ni mlima wa nne kwa urefu Tanzania katika ya milima mirefu 25 iliyopo Tanzania. Mlima huu una urefu wa mita 3,648 unapatikana katika mkoa wa Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania.


Mlima Shira, mita 3,626 (Kilimanjaro)

Mlima Shira wenye urefu wa mita 3,626 ni miongoni mwa vilele vitano Tanzania. Mlima huo uliopo mkoani Kilimanjaro unatofautiana mita 22 tu na Mlima Lool Malasin.

Mlima Oldeani, mita 3,188 (Arusha/Manyara)

Mlima Oldeani unaopatikana katika mikoa miwili ya Manyara na Arusha una urefu wa mita  3,188 na kuufanya kuwa mlima wa sita kwa urefu nchini. Tofauti na milima maarufu ya Kilimanjaro na Meru, hakuna taarifa nyingi za kina kuhusu Mlima Oldeani.


Mlima Hanang, mita 3,103 (Manyara)

Mlima Hanang ni mlima unaoshika nafasi ya saba kati ya milima kumi mirefu zaidi Tanzania ukiwa na mita 3103. Mlima huu unapatikana katika mkoa wa Manyara ukiwa ni tofauti ya mita 1,463 na Mlima Meru unaopatikana mkoani Arusha. 


Jaeger, mita 3,050 (Arusha)

Jaeger ni mlima wa nane katika orodha milima mirefu zaidi nchini. Mlima huu wenye urefu wa mita 3,050 unapatikana katika mkoa wa Arusha. Jaeger ni mlima wa nne kwa urefu mkoani humo baada ya milima Meru, Oldeani na Hanang. Tofauti na Mlima Meru, Jaeger hauna taarifa za kutosha za kuwasaidia watalii kujua kwa undani namna ya kutalii.


Monduli, mita 3,000 (Arusha)

Mlima Monduli una mita 3,000 upo katika mkoa wa Arusha ukiwa ni mlima wa tisa kwa urefu nchini. Huu ni mlima wa tano kwa urefu Arusha. Hii ina maana iwapo unataka kuvunja historia, unaweza kuipanda milima yote mkoani humo ukawa umeshapanda milima mitano kati ya 10 mirefu zaidi nchini. 


Mtorwi, mita 2,961 (Njombe)

Watu wengi hudhani mlima Rungwe ni moja ya milima yenye vilele virefu zaidi hii ni kutokana na umaarufu wake lakini takwimu za NBS zinaonyesha tofauti. Rungwe unazidiwa urefu wa mita moja tu na Mlima Mtorwi kutoka mkoa Iringa ambao ndiyo mlima wa 10 kwa urefu Tanzania. Mtorwi wenye mita  2,961 ndiyo kilele cha Nyanda za Juu Kusini. Mlima Mtorwi ni sehemu ya platu ya Kitulo ambayo ni maarufu kutokana na maua yake. 

Hata hivyo, mtandao wa lonelyplanet unasema miundombinu ya upandaji mlima hususan wakati wa masika siyo mzuri hivyo ni bora wapandaji wakafanya utalii wakati wa kiangazi. 

Kilele cha Mlima Mtorwi mkoani Njombe. Huu ni mmoja ya milima ambayo taarifa zake hazipatikani kirahisi mtandaoni. Picha|Google Maps.

Related Post