Bajeti ya Muungano na Mazingira yapaa kwa Sh6.3 bilioni

Lucy Samson 0618Hrs   Aprili 23, 2024 Habari
  • Bajeti yafikia Sh45.7 kutoka Sh39.3 iliyoidhinishwa mwaka wa fedha 203/24.
  • Bajeti pia itasaidia mradi wa kuhimiri athari za mafuriko jijini Dar es Salaam na Zanzibar.


Dar es Salaam. Huenda shughuli za maendeleo pamoja na uhifadhi wa mazingira zinazofanywa na Wizara ya Muungano na Mazingira zikaimarika zaidi katika mwaka ujao wa fedha ikiwa Bunge litaidhinisha Sh45.7 bilioni zilizoombwa na wizara hiyo.

Bajeti hiyo ya 2024/25 imeongezeka kwa asilimia 16.1 kutoka Sh39.3 bilioni zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2023/24 unaoisha Juni mwaka huu.

Waziri wa wizara hiyo iliyopo Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Selemani Jafo ameliambia Bunge leo Aprili 23, 2024 jijini Dodoma kuwa kati ya fedha hizo Sh23.8 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh21.9 bilioni ni matumizi ya miradi ya maendeleo.

“Matumizi ya kawaida yanajumuisha Sh3.8 bilioni na 5.8 bilioni mishahara ya Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc) na Sh14.9 bilioni matumizi mengineyo,” amesema Waziri Jafo.

Ikiwa fedha hizo zitaidhinishwa Waziri Jafo amesema wizara yake itaweza kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa kuhimiri athari za mafuriko na kuongezeka kwa usalama chakula katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko jijini Dar es Salaam na Zanzibar.


Soma zaidi:Tamisemi yaomba kuidhinishiwa Sh10 trilioni mwaka wa fedha 2024-25


Mingine ni miradi wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ya Halmashauri ya Magu, mkoani Mwanza,  Nzega mkoani Tabora na Mkalama mkoani Singida pamoja na mradi wa kuandaa mkakati wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kuhifadhi Bianuai 2025/30

Kutekelezwa kwa miradi hiyo kutaisaidia Tanzania katika mapambano ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mabadiliko ya kunyesha kwa mvua na mafuriko yaliyoharibu miundombinu na kusababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha.

Hivi karibuni Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Mahinyi, aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam amesema mpaka kufikia Apili 15, 2024 jumla ya watu 33 wamepoteza maisha kutokanana mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Pwani na Morogoro

Watu 5 walipoteza maisha wilayani Rufiji mkoani Pwani huku wengine 28 wakipoteza maisha mkoani Morogoro.

Athari nyingine ni kuharibika kwa mazao ya chakula kama mahindi, mpunga, ufuta mihogo, mtama na pamba pamoja na miundombinu ikiwemo makazi, madaraja, nguzo za umeme na barabara.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kuendelea kwa mvua za El-nino katika baadhi ya maeneo nchini jambo linaloashiria kuhitajita kwa fedha zaidi kuhudumia waathirika na kuimarisha miundombinu.

Vipaumbele vya wizara

Vipaumbele vya Wizara ya Muungano na Mazingira kwa mwaka 2024/25 kuwa ni kuratibu vikao ya kamati muungano, kuanzisha Kituo cha Kumbukumbu za Nyaraka za Muungano na kuratiibu masuala ya kiuchumi na kijamii.

Vipaumbele vingine ni kutoa elimu kwa umma kupitia redio, luninga, mijadala, magazeti na machapisho, kushiriki katika maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Muungano pamoja na kuandaa programu za mifumo ya kielektroniki ya kuratibu masuala ya Muungano na yasiyo na Muungano.

Related Post