Bajeti ya kilimo yapaa kwa miaka mitano mfululizo

Lucy Samson 0842Hrs   Mei 02, 2024 Habari
  • Yafikia Sh1.24 trilioni kwa mwaka 2024/25.
  • Kamati yasema fedha hizo hazitoshelezi mahitaji ya wizara.
  • Waziri aanika vipaumbele sita ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa masoko.


Dar es Salaam.Huenda sekta ya kilimo nchini Tanzania ikapata msukumo mpya wa maendeleo na kuongeza mchango wake katika uchumi mara baada ya kushuhudiwa ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa miaka mitano mfululizo.

Bajeti ya Wizara ya Kilimo imekuwa ikipaa kwa miaka mitano mfululizo kutoka Sh229.83 bilioni mwaka 2020/21 na kufikia Sh1.24 trillioni mwaka 2024/25 jambo linalotazamiwa kuleta matokeo chanya kutokana na asilimia kubwa ya fedha hizo kuelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Bajeti iliyoombwa na Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2024/25 imepaa kwa Sh278.1 bilioni sawa na asilimia 26.8 ya Sh970.7 bilioni iliyoidhinishwa mwaka 2023/24.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe  aliyekuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni jijini Dodoma leo Mei 2, 2024 amewaambia wabunge kati ya fedha hizo Sh700.3 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Katika mwaka 2024/25, Sh824,069,158,000 zinaombwa. Kati ya fedha hizo Sh700,318,469,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo Sh194,525,642,532,000 ni fedha za ndani na Sh174,675,937,000 ni fedha za nje,” amesema Waziri Bashe.

Kuongezeka kwa bajeti hiyo kwa mwaka 2024/25 kunaifanya wizara hiyo kuweka rekodi ya kuongezeka kwa bajeti yake ndani ya kipindi cha miaka mitano mfululizo tangu ilipoanza kupaa mwaka 2020/21.


Soma zaidi:Mustakabali wa kikokotoo cha mafao bado kizungumkuti Tanzania


Vipaumbele vya mwaka 2024/25

Kwa mwaka 2024/25 Wizara ya Kilimo imekusudia kutekeleza vipaumbele sita ikiwemo kuongeza tija na uzalishaji, kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo.

Vingine ni kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya mazao nje ya nchi, kuimarisha maendeleo ya ushirika na kuimarisha  matumizi ya mifumo ya Tehama(Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) katika uendelezaji wa sekta ya kilimo.  

Fedha bado hazitoshi

Licha ya Serikali kuogeza fedha za wizara hiyo kwa miaka mitano mfululizo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema fedha hizo hazitoshelezi mahitaji ya wizara kwa kuzingatia azimio la Maputo la mwaka 2003 na Malabo la mwaka 2014.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile aliyekuwa akiwasilisha maoni hayo amesema maazimio hayo yanatoa masharti kwa nchi zote wanachama kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti yote ya Serikali kwa ajili ya Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi zilizo chini yake.


Uchambuzi wa Bajeti ya Serikali unabainisha kuwa Wizara ya Kilimo imetengewa asilimia 2.4 tu ya bajeti kuu kati ya  Sh49.3 trilioni zilizotengwa.

Aidha, kamati hiyo imeishauri Serikali kutoa fedha zilizoidhinishwa kwa wizara hiyo kwa wakati ili kurahisisha shughuli za maendeleo pamoja na kuongeza nguvu katika uzalishaji wa pembejeo za kilimo.

“Kamati inaishauri Serikali kuongeza nguvu na kuchukua hatua za makusudi za kuzalisha pembejeo hapa nchini ikiwemo mbolea, mbegu na viwatilifu,”

Pia ameitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa  pembejeo hizo ili waweze kupata tija katika uzalishaji wa mazao.

Related Post