‘Dada poa’ 18 wadakwa kwa kujiuza Mwanza

Mariam John 0831Hrs   Mei 02, 2024 Habari
  • Ni wale waliokuwa wakijiuza katika eneo la Shule ya Msingi Kitangiri A iliyopo Ilemela mkoani Mwanza.
  • Jeshi la Polisi laonya vitendo hivyo, kuwasaka wanunuaji.


Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia wanawake 18 waliokutwa wanafanya biashara ya kuuza miili yao ili kujipatia kipato katika eneo la Shule ya Msingi Kitangiri A iliyopo Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema wanawake hao wamekamatwa mwishoni mwa mwezi Aprili wakijihusisha na vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili na wamefikishwa katika Mahakama ya  Mwanzo Ilemela.

Kamanda Mutafungwa amewataja watu hao kuwa ni Amina Bakari (33) mkazi wa mtaa wa Ghana Ilemela, Zawadi Richard (20) mkazi wa Usagara, Ashura Hamis (17) mkazi Nyamanoro, Mary Revinus mkazi wa Bwiru, Beatrice Nyanda, mkazi wa Nyakato Natinal, Hamisa Hamis, mkazi wa Mkundi na Fetty Aron mkazi wa Kirumba

Wengine ni Victoria Michael mkazi wa mtaa wa Ibada, Sara Seleman mkazi wa Nyamanoro, Monica Jacob mkazi  mkazi wa Kitangiri, Rosemary Leonard mkazi wa Ibanda, Kiza Adam mkazi wa Nyegezi, Koku Samson mkazi wa Kabuhoro, Neema Jovin mkazi wa Nyang’omango, Joyce Patric mkazi wa Kirumba, na Joyce Sinsi mkazi wa Kiseke na Mariam John mkazi wa Mabatini.

“Mara kadhaa sasa, wanawake hao wamekuwa wakikamatwa na kupewa adhabu mbalimbali lakini vitendo hivyo havikomi vimekuwa vya kujirudia,” amesema Mutafungwa.


Soma zadi:Mustakabali wa kikokotoo cha mafao bado kizungumkuti Tanzania


Suala la ‘dada poa’ kutumia maeneo ya shule zisizo na uzio kwa ajili ya kujiuza ni miongoni mwa hoja zilizoibua mjadala bungeni siku za hivi karibuni.

Aprili 23, mwaka huu Mbunge wa Ilemela, Angelina  Mabula alihoji Shule ya Msingi Kitangili kutumika na ‘dada poa’ kujiuza nyakati za usiku hali inayohatarisha usalama wa watoto ambao wakati wa mchana wakiwa shuleni huchezea mipira ya kiume (kondomu) ambazo hutupwa na kuzagaa uwanjani.

Katika majibu yake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilemela kwenda katika shule hiyo na kufanya tathimini ili kujenga uzio utakaokuwa muarobaini wa vitendo hivyo.

“Kuna kila sababu ya halmashauri kupita mapato yake ya ndani na kutenga fedha kwa ajili ya kujenga uzio huo ili kunusuru na kutengeneza mazingira bora ya watoto wetu,” amesema Katimba.

Aidha, Mutafungwa amewataka wanawake kuacha tabia ya  kufanya vitendo hivyo badala yake wajiingize kwenye shughuli za kihalali za kujiingizia kipato kuliko  hivi wanavyofanya sasa ambavyo ni kinyume na maadili lakini pia vina madhara kiafya.

Pia Kamanda huyo amewataka wanaume kuacha tabia ya kununua akina dada wa aina hiyo ili wasiendelee kuchochea vitendo hivyo.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Asha Seleman mkazi jijini Mwanza aliyeiomba Serikali kuwachukulia hatua kali wote wanaojiuza na wanaonunua ili kukomesha kabisa vitendo hivyo.

Related Post