Bunge: Serikali itoe muongozo kudhibiti mikopo ‘kausha damu’

Sayuni Kisige 0926Hrs   Mei 02, 2024 Habari
  • Serikali yasema itafanya semina ya wabunge na taasisi za fedha kukusanya maoni.
  • Mrejesho kutolewa Bunge la Septemba.

Dar es salaam. Bunge la Tanzania limeitaka Serikali kupitia upya miongozo ya utoaji wa huduma ya mikopo kwa kampuni na taasisi zinazotoa huduma hiyo na kisha  kutoa muongozo utakaodhibiti kutoza viwango vikubwa vya riba kwa wakopaji ili kudhibiti mikopo ‘kausha damu’.

Uamuzi huo wa Bunge unakuja wakati ambao kwa muda sasa jamii imekuwa ikilalamika juu ya uwepo wa mikopo hiyo ambapo mkopaji hulazimika kurejesha mkopo kwa riba kubwa ndani ya muda mfupi na baadhi ya wakopaji hujikuta wakiuza au kuchukuliwa mali zao pale wanaposhindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Aprili 24, 2024, Felista Njau ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliitaka Serikali kutoa majibu juu ya namna ya  kudhibiti riba za mikopo hiyo ambayo kwa mujibu wake imeathiri wananchi wa maeneo mengi nchini.

Katika swali la msingi, mbunge huyo ametaka kujua kuna mkakati gani ya kufuatilia na kuchukua hatua kwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye riba kubwa kinyume na muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).



Soma zaidi: Bajeti ya kilimo yapaa kwa miaka mitano mfululizo


“Mheshimiwa spika taasisi zingine zina ofisi, zina leseni mfano mikopo iliyoandikwa 'One Answer', Kausha Damu, Kichefuchefu, wanachaji asilimia 60 mpaka 80…

…mikopo hii unarejesha kila siku Sh22,000 kwa siku mpaka ikifika tarehe 30, ukivusha siku moja hujapeleka wanakuja na gari wanabeba kitanda, godoro na kila kitu”, amebainisha Njau.

Aidha, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Shally Raymond, amesema pamoja na Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  ya mwaka 2018 na Kanuni za Mwaka 2019, takribani mikoa 17, ukiwamo Kilimanjaro hasa Wilaya ya Moshi, imekuwa ikitolewa mikopo kausha damu na kutaka kauli ya Serikali. 

“Kampuni za simu zimekuwa zikitoa mikopo haraka bila kujaza fomu na vijana na wanawake wajasirimali wa Kilimanjaro wamekuwa wakichangamkia fursa hiyo, Je? lini serikali italazimisha kampuni hizo kutoa elimu?” alihoji Raymond.


/span>


Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba aliyekuwa akitoa majibu ya maswali hayo leo Mei 2, 2024 bungeni jijini Dodoma amewaambia wabunge kuwa Serikali imechukua jambo hilo na inaenda kulifanyia kazi kwa kina.

“Ili tuweze kuboresha zaidi, nitafanya semina ya wawakilishi wa wanachi na taasisi za kifedha ili tukubaliane kuhusu jambo hili…. Tukubaliane ili wabunge waziambie taasisi zangu zote namna gani wanataka sheria zisimamie maslahi ya wananchi wanaowawakilisha,” amesema Nchemba.

Nchemba amesisitiza kuwa ikiwezekana jambo hilo litafanyika katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti linalotarajiwa kutamatika Juni 30, 2024.

Hata hivyo, Spika wa Bunge la Tanzania Dk. Tulia Ackson amesema kuwa kutokana na unyeti wa jambo hilo, wananchi watarajie kusikia majibu kutoka Serikalini katika Bunge lijalo la Mwezi Septemba.

“Maadam tupo hapa kwenye hiki kipindi watumie muda mwingi kuwasikiliza wabunge maadam tupo hapa, na baadae wakawasikilize wananchi kwa kuwa athari ni kubwa, halafu tutasikia kama watakuwa wamepiga hatua yoyote kwenye Bunge la mwezi wa tisa,” amesema Dk. Tulia. 

<

Related Post