Wanafunzi 25,532 elimu ya juu wapata mikopo awamu ya kwanza

Daniel Samson 0959Hrs   Oktoba 17, 2018 Habari
  • Orodha iliyotolewa leo ni ya kwanza lakini mchakato wa kuwapangia wanafunzi mikopo utaendelea kulingana na uhitaji na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni.
  • Dirisha la kukata rufaa kufunguliwa Novemba 1 hadi 15, 2018 kwa wanafunzi ambao hawajapata au hawajaridhika na kiwango cha mikopo walichopangiwa.

Dar es Salaam. Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) imetangaza orodha ya kwanza ya majina ya  wanafunzi 25,532 katika ya 40,285 wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo kwaajili ya mwaka wa masomo wa 2018/2019.  

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razak Badru amesema orodha iliyotolewa leo ni ya kwanza lakini mchakato wa kuwapangia wanafunzi mikopo utaendelea kulingana na uhitaji na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni.

“Wanafunzi 25,532 kati ya 40,285 wamepangiwa mikopo na mikopo hii waliyopangiwa ina thamani ya bilioni 88.36 mpaka sasa tulivyopanga katika awamu hii ya kwanza. Wanafunzi hawa wamegawanyika kama ifuatavyo hao wa mwaka wa kwanza wakiume wako 16,085 na wa kike wako 9447,” amesema Badru. 

Amesema mwaka huu Serikali iliidhinisha jumla ya Sh427.5 bilioni kwaajili ya kuwapangia wanafunzi wapatao 123,285 wa elimu ya juu ikijumuisha wale wanaoendelea na wa mwaka wa kwanza ambao wanatarajia kuanza masomo yao Novemba, 2018.  

“Leo tumekamilisha awamu za uchambuzi na baada ya orodha ya udahili kutoka kwenye Tume ya Vyuo vikuu (TCU) na sisi tumeendelea kuchakata zile taarifa, kulinganisha taarifa walioomba mikopo na wale waliopata vyuo,” amesema.

Amesema licha ya wanafunzi wengi kuomba mikopo, wapo ambao hawajadahiliwa katika vyuo ambapo hawawezi kupata mikopo mpaka wapate orodha kutoka TCU inayothibitisha kuwa wanafunzi hao wamedahiliwa katika vyuo vinavyotambulika na Serikali.

“Pamoja na kuomba mkopo lazima uwe umedahiliwa katika chuo kinachotambulika na Serikali na ndio maana unaona taarifa hii ya udahili kutoka TCU inakuwa muhimu sana kutuwezesha sisi kupanga mikopo,” amesema.

Aidha, HESLB inakusudia kufungua dirisha la kukata rufaa Novemba 1 hadi 15, 2018 kwa wanafunzi ambao hawajapata au hawajaridhika na kiwango cha mikopo walichopangiwa katika awamu ya kwanza. 

Rufaa hiyo itahusisha wanafunzi kutoka katika orodha ya ya waliodahiriwa iliyopokelewa kutoka TCU mpaka sasa ambayo inafikia wanafunzi 49,000.

Fedha hizo Sh88.6 bilioni ni kati ya fedha zote zilizotengwa kwaajili ya bajeti ya kuwapangia wanafunzi  kulipia mikopo katika robo ya kwanza ya mwaka 2018/2019 ikizingatiwa kuwa fedha hizo zinalipwa kwa mkupuo kutoka hazina.


Zinazohusiana: HESLB kuboresha mfumo wa utoaji, urejeshaji mikopo elimu ya juu.


Mkopo huo pia utajumuisha wanafunzi 69 wanaosoma katika vyuo vya nje ambavyo Serikali inapata ufadhili kutoka Serikali rafiki katika nchi za Msumbiji, Algeria, Cuba, Urusi, Sebya na Ujerumani  ambapo thamani ya mkopo wao ni Sh800.35 bilioni.

Baada ya kukamilisha awamu ya kwanza itatangazwa awamu ya pili ya wanafunzi wanaostahili kupata mikopo hiyo ambapo itazingatia orodha ya udahiLi kutoka TCU na sifa zinazopo kwenye miongozo na vigezo ya bodi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB, Dk Veronica Nyahende amesema wanafunzi 83,000 wanaotendelea na masomo nao wana nafasi ya kupata mkopo kwa mwaka 2018/2019 ambapo hupangiwa mkopo baada ya kupata matokeo yakionyesha mwanafunzi amefaulu na anaendelea na masomo.

“Mpaka sasa vyuo karibu 10 havijaleta matokeo kwa maana hiyo wanafunzi wa vyuo hivyo wanaweza kuchelewa kupata pesa zao. Matokeo yanatakiwa yaletwe siku 30 kabla chuo kufunguliwa na kwa wale ambao wanarudia wanafanya supplementary (wanarudia mtihani) yanatakiwa kufikishwa siku 30 baada ya vyuo kufunguliwa,” amesema Dk Nyahende.

Dirisha la kuomba mkopo katika bodi ya HESLB kwa wanafunzi waliokuwa wanatarajia kujiunga na vyuo mwaka huu lilifunguliwa Mei 2018 na likafungwa Agosti 10, 2018, ambapo wamepokea maombi ya waombaji mikopo zaidi ya 76,000

Related Post