Kimbunga Hidaya chazidi kusogea zaidi Tanzania, Temesa yasitisha vivuko

Esau Ng'umbi 0320Hrs   Mei 04, 2024 Habari
  • Kipo karibu na maeneo ya mkoa wa Lindi, Pwani, na Dar es Salaam.
  • Kinatarajiwa kupungua nguvu usiku wa kuamkia kesho Jumapili Mei 5, 2024
  • Upepo wake una kasi ya kilomita 120 kwa saa
  • Wananchi waonywa kuendelea kufuatilia taarifa kutoka TMA na kuchukua tahadhari


Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijiandaa kukabiliana na athari za kimbunga Hidaya kilichotarajiwa kuwasili nchini kuanzia usiku wa Mei 3, 2024 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga hicho kuwa kipo karibu na maeneo ya pwani ya nchi kwa umbali usiozidi kilomita 130. 

Kwa mujibu wa TMA hadi kufikia majira ya saa tisa usiku wa kuamkia leo, Kimbunga Hidaya kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa mkoani Lindi, kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia (Pwani)  na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.

Kasi ya kimbunga hicho ni ya juu zaidi ya ukomo unaoshauriwa wa kuendesha gari wa kilomita 80 kwa saa.

“Uwepo wa kimbunga "HIDAYA" karibu kabisa na pwani ya nchi yetu umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa katika maeneo hayo, ambapo katika kipindi cha masaa 6 yaliyopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza. 

…Mfano katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umepimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii,” imebainisha taarifa ya TMA iliyotolewa Mei 4 saa 3 asubuhi.


Soma zaidi: Mvua, mafuriko vyaua watu 161 Tanzania, Serikali ikionya kimbunga Hidaya


TMA wameongeza kuwa katika kipindi hicho, vipindi vya mvua kubwa vimeendelea kushuduhiwa katika maeneo ya Mtwara na Lindi ambapo hadi kufikia saa 9 usiku kituo cha Mtwara kiliripoti jumla ya milimita 75.5 za mvua ndani ya masaa 12. 

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wameripoti kuwepo upepo katika maeneo yao wengine wakichapisha kwenye mitandao video namna miti inavyotikiswa na upepo. 

“Kiwango hiki cha mvua ndani ya masaa 12 ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Mtwara ni milimita 54 tu. Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 12 katika kituo cha Mtwara ni takribani asilimia 140 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Mtwara,”  TMA imeeleza.


Bofya hapa kufuatilia kimbunga live


Kimbunga kuendelea kusogea 

Taarifa ya TMA imesema Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya Tanzania huku kikipungua nguvu yake taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili ya  tarehe 05 Mei 2024.

Katika kipindi hicho kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa Pwani hususan mikoa ya Lindi Mtwara, Pwani na Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani  ambapo matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.

Chukua tahadhari

TMA imewataka wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari kubwa pamoja na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka mamlaka husika na taasisi za Serikali ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa mali pamoja na vifo.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa Kimbunga Hidaya na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi,” imesema TMA.



Huduma ya vivuko yasimamishwa

Kutokana na uwepo wa tahadhari ya Kimbunga Hidaya katika maeneo ya Pwani ya Tanzania, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa)  umesitisha utoaji wa huduma ya vivuko katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Mkoa wa Dar es Salaam na Tanga.

Temesa imebainisha kuwa imefikia uamuzi huo ili kujilinda na kuepukana na athari zozote ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na Hidaya na kusababisha athari kwa watumiaji wa vivuko.

“Temesa inaendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ili kuhakikisha abiria wote wanaotumia huduma hizo wanakuwa salama wakati wote,” imebainisha taarifa ya Temesa iliyochapishwa katika kurasa za mitandao ya kijamii.

Related Post