Kimbunga Hidaya chawatesa wavuvi nane baharini Dar es Salaam

Esau Ng'umbi 1102Hrs   Mei 04, 2024 Habari
  • Wakwama baharini usiku wa manane, matanga yakiharibiwa na upepo
  • Sita waokolewa usiku, mmoja apatikana asubuhi
  • Waahidi kuchukua tahadhari baada ya kunusurika kifo 


Dar es Salaam. Wavuvi wanane wanaofanya shughuli zao  jijini Dar es Salaam watabaki na historia ya madhara ya kimbunga Hidaya baada ya upepo mkali kuharibu vyombo vyao katikati ya bahari wakivua samaki.

Wavuvi hao licha ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuwataka watumiaji bahari kuchukua tahadhari kutokana na madhara ya kimbunga hicho, wavuvi hao walijitosa kwenda kuvua kama siku za kawaida.

Wakiwa baharini usiku wa jana (Mei 3, 2024) upepo mkali na mawimbi yalivyoruga shughuli ya wavuvi hao wenye kambi yao katika ufukwe wa Kawe jijini hapa.

Mashuhuda wa tukio wameiambia Nukta Habari kuwa wavuvi hao walikwama kwa zaidi ya saa tatu baharini hadi walipokuja kuokolewa na wenzao wenye vyombo vyenye injini.

Hamis Mtega, Mvuvi katika fukwe ya Kawe ambaye alishiriki katika zoezi la uokozi, ameiambia Nukta Habari kuwa licha ya kufahamu kuhusu tahadhari iliyotolewa wavuvi wengi waliendelea na shughuli zao kama kawaida jambo lililowaweka hatarini wavuvi nane kutokana na vyombo vyao kushindwa kuhimili upepo mkali.

“Kulikuwa na vyombo sita vilivyokwama, na vingi viliharibika kwa sababu vyombo vyetu vingi sio mashine, kwa hiyo yale matanga yalichanika na milingoti yake ilikatika. Sisi wenye mashine  tukapambana tukawasaidia tukawatoa, ila kuna mmoja hatukumuona kabisa,” amesema Mtega.

Mtega amebainisha kuwa mtu mmoja amepatikana asubuhi katika fukwe ya Kunduchi baada ya kuokolewa na wavuvi wanaovua katika ukanda huo.


Nini hutokea mtu akipotea baharini

Kwa mujibu wa Mtega ambaye ni mvuvi kwa zaidi ya miaka 10, chombo kinapoharibika majini upepo na nguvu ya maji ndio huamua uelekeo wa chombo hicho.

“Watu huwezi  kuwakuta pale walipofikia, inategemea upepo unawapeleka sehemu gani, wenyewe ndo unaamua na uwezo wa kurudi unakuwa haupo ni mpaka kipite chombo kikubwa wapate msaada vinginevyo wanalala baharini,”  Mtega ameeleza.


Soma zaidi: Kimbunga Hidaya chazidi kusogea zaidi Tanzania, Temesa yasitisha vivuko


TMA ilionya mapema

Wakati wavuvi hao nane wakinusurika kifo kutokana na Kimbunga Hidaya, TMA ilionya mapema juu ya kimbunga hicho ikibainisha kuwa kitabadili na kutawala mfumo wa hali ya hewa na kuleta madhara ukiwemo upepo mkali na vipindi vya mvua kubwa mikoa ya Pwani ikiwemo ya Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro, Pemba, Unguja na Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Umoja wa wavuvi wa Fukwe Kawe, Mudu Mbegu amesema baadhi ya wavuvi huwa wana tabia ya kubishia mamlaka ukiwemo utabiri wa hali hewa. 

“Wavuvi tuliwarudisha jana saa saba usiku walienda kutega sehemu moja inaitwa Fungu ya Sini upande wa Kaskazini kama unaelekea Unguja, kulikuwa na ngalawa tano, na mitumbwi mitatu ambayo yote imeokolewa,” amebainisha Mbegu.

Kiongozi huyo anasema walipokea taarifa ya uwepo wa kimbunga hicho tangu Mei 2, 2024 na baadhi yao walichukua tahadhari huku wengine wakipuuza.


Bofya hapa kufuatilia kimbunga live


Maandalizi ya uvuvi yanaendelea, tahadhari imechukuliwa

Licha ya taarifa ya TMA iliyotoka saa tatu asubuhi leo Mei 4, 2024 kubanisha kuwa  mwenendo wa kimbunga Hidaya kipo karibu na maeneo ya pwani ya nchi kwa umbali usiozidi kilomita 130 kikiwa na kasi inayozidi kilomita 120 kwa saa, mwandishi wa Nukta Habari ameshuhudia wavuvi wa eneo hiko wakiendelea na maandalizi ya shughuli zao ikiwemo kushona nyavu.

Alipoulizwa iwapo wana mpango wa kuvua leo licha ya hatari, Mbegu amebainisha kuwa tahadhari waliyochukua ni kutokwendaa kutega katika maeneo ya mbali na fukwe ili iwe rahisi kukabiliana na changamoto yoyote itakayojitokeza.

“Watu tunazidi kuwaelekeza, pamoja na maandalizi yao tunawaambia tahadhari zizingatiwe, kitakachofanyika hawa hawataenda kutega tena mbali, watatega humu humu wakiona hali mbaya watasubiri mpaka kipungue lakini hawatoenda mbali kwa sababu wameshaziona athari zake,” amesema Mbegu.


Soma zaidi: Mvua, mafuriko vyaua watu 161 Tanzania, Serikali ikionya kimbunga Hidaya


Kwa mujibu wa TMA hadi kufikia majira ya saa tisa usiku wa kuamkia leo, Kimbunga Hidaya kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa mkoani Lindi, kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia (Pwani)  na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa.

Kasi ya kimbunga hicho ni ya juu zaidi ya ukomo unaoshauriwa wa kuendesha gari wa kilomita 80 kwa saa.

“Uwepo wa kimbunga "HIDAYA" karibu kabisa na pwani ya nchi yetu umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa katika maeneo hayo, ambapo katika kipindi cha masaa 6 yaliyopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza. 

…Mfano katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umepimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii,” imebainisha taarifa ya TMA.

Kimbunga kuendelea kusogea 

Taarifa ya TMA imesema Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya Tanzania huku kikipungua nguvu yake taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 05 Mei 2024.

Katika kipindi hicho kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa Pwani hususan mikoa ya Lindi Mtwara, Pwani na Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani  ambapo matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.

Related Post