Mvua, mafuriko vyaua watu 161 Tanzania, Serikali ikionya kimbunga Hidaya

May 3, 2024 4:45 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Watu 161 wamefariki dunia ndani ya mwezi mmoja kutokana na athari za mafuriko na mvua kubwa za El-nino zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini wakati Taifa likijiandaa kukabiliana na madhara ya kimbunga Hidaya kinachotokea mashariki mwa bahari ya Hindi.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amewaambia wanahabari jijini Dodoma kuwa mbali na vifo hivyo, zaidi ya watu 250 wamejeruhiwa kutokana na maafa hayo yaliyoathiri takriban nchi nzima.

Matinyi amesema hadi leo Mei 3, 2024 kaya 52,000 zimeathirika na maafa hayo zikiwa na watu zaidi ya 210,000.

 “Zaidi ya nyumba 15,000 zimeathirika na majeruhi mpaka sasa ni zaidi ya watu 250 na maeneo ambayo yametajwa kuguswa na maafa hayo ni mkoa wa Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Kigoma, Iringa, Tabora, Dodoma, Lindi, Arusha na Mtwara,” Matinyi amesema leo katika mkutano wake na wanahabari.

“Pia, maafa yamegusa Kagera, Shinyanga, geita, Songwe, Rukwa, na Manyara, karibu nchi nzima.”

Kwa zaidi ya mwezi sasa Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya zimekuwa zikikabiliwa na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko, maporomoko ya udongo na athari nyingine zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.

Nchini Kenya Rais William Ruto ameeleza kuwa hadi sasa watu wasiopungua 210 wamefariki dunia ndani ya wiki za hivi karibuni na kwamba na hali inatarajiwa kuwa mbaya katika mwezi mmoja ujao.

Matinyi amesema Serikali inaendelea kuwahudumia waathirika wa maafa hayo huku akiwasihi Watanzania kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa na kuepuka maeneo ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao.

Tanzania kuanzia usiku wa leo inajiandaa kukabiliana na madhara ya kipunga kikali kiitachwo Hidaya ambacho kinatarajia kubadili mfumo wa hali ya hewa na kuleta madhara ukiwemo upepo mkali na vipindi vya mvua kubwa mikoa ya Pwani ikiwemo ya Lindi, Mtwara, Pwnai, Morogoro, Pemba, Unguja na Dar es Salaam.

“Vipindi vya mvua na upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa sasa tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Lindi na Mtwara hadi kufikia Saa 9 mchana siku ya leo nikimaanisha katika maeneo ya nchi kavu ndani ya nchi yetu,” amesema.

Matinyi amewaonya watumiaji wa bahari kufuata maelekezo ya kuepuka na madhara ya kimbunga hicho ambacho Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) inategemea kuwa nguvu yake itakuwa imepungua kidogo.

Enable Notifications OK No thanks