Rais Samia: Kuna nyongeza ya mishahara mwaka huu

May 1, 2023 11:34 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, K Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Profesa Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Tumaini Nyamhokya pamoja na Viongozi wengine wakiimba Wimbo wa Mshikamano (Solidarity) wakati wa Sherehe ya Mei Mosi ambazo Kitaifa zimefanyika uwanja wa Jamhuri – Morogoro. Picha | Ikulu.


  • Wafanyakazi kuanza kupata mwaka huu. 

  • Serikali itaboresha zaidi maslahi ya wafanyakazi uchumi ukiruhusu.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amerejesha utaratibu wa nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma ya kila mwaka ambao ulisitishwa kwa muda mrefu na ameahidi nyongeza hiyo itaanza kutolewa mwaka huu wa 2023.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Mei Mosi 2023 mkoani Morogoro katika sherehe za maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani amesema utaratibu huo utaanza mwaka huu.

 “Niseme pia kuna nyongeza za mishahara kwa mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa nikaona mwaka huu tuzirudishe.

“Kwa hiyo wafanyakazi wote mwaka huu mbali niliyoyasema lakini kuna nyongeza za mishahara kila mwaka na tunaanza mwaka huu na tutaenda kila mwaka kama ilivyokuwa hapo zamani,” amesema Rais Samia. 

Hata hivyo, kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema Serikali haiwezi kutaja hadharani nyongeza hiyo ya mshahara ili kuepuka kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali sokoni kunakowezwa kufanywa na baadhi ya watu.

“Kile watu walichozoe tukisema hapa ili wapandishe bei madukani mara hii hakuna tunakwenda polepole kupandishana kama tulivyosema, wasione tumeongezeana kitu gani ili mwenendo wetu wa bei uwe salama,” amesema Rais Samia. 

Amewataka wafanyakazi kutokuwa na wasiwasi kwa sababu “mambo mazuri yapo lakini hatutayatangaza hapa (kwenye sherehe za Mei Mosi) lakini wafanyakazi mambo ni moto, mambo ni fire.”

Rais Samia hajatangaza kupunguza kodi ya mishahara na kuongeza kima cha chini cha mishahara kama alivyofanya mwaka jana mpaka pale uchumi utakaporuhusu huku akiahidi kuboresha posho za wafanyakazi.

“Tulipandisha posho za wafanyakazi na waliofaidika na hili ni wafanyakazi wenye mishahara mikubwa ambao hawakufaidika na asilimia 23 (nyongeza ya mshahara). Mwaka huu kuna mavuno makubwa upandishaji wa viwango vya posho vitapatikana,” amesisitiza Rais.


Soma zaidi: 


Akizungumzia kuhusu ukataji wa kodi ya marupurupu ya wafanyakazi, changamoto za bima ya afya, malimbikizo ya madeni ya mishahara na mafao ya  watumishi yaliyoibuliwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Heri Mkunda,  amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na watendaji wengine wa Serikali washughulikie ili ipatikane suluhu.

Licha ya changamoto lukuki za wafanyakazi, Rais Samia amewaahidi wafanyakazi kuendelea kuboresha mazingira na sheria za kazi ili kuhakikisha watumishi wa umma na sekta binafsi wanapata maslahi bora na kuboresha maisha yao.

Tucta watoa ya moyoni

Katibu Mkuu wa TUCTA, Heri Mkunda akitoa risala ya wafanyakazi kwa Rais Samia amempongeza kwa kutekeleza ahadi ilizozitoa katika sherehe za Mei Mosi mwaka jana ikiwemo kuongeza nyongeza ya mshahara na kupunguza kodi ya mshahara.

Hata hivyo, Mkunda amemuomba Rais Samia kuongeza posho na marupurupu kwa wafanyakazi, jambo litakalosaidia kuongeza kipato cha watumishi wa umma ili waweze kupunguza ukali wa maisha.

“Tunaendelea kukuomba ili kupata ajira za staha katika sehemu zetu za kazi tunaomba Serikali itusaidie kuboresha kitengo cha idara ya kazi ambacho kiko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ambacho kina wafanya kazi wachache,” amesema Mkunda. 

Maombi mengine ni malimbikizo ya madeni ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi wa afya na kupunguza au kuondoa kabisa kodi inayokatwa kwenye marupurupu nje ya mshahara.

“Tunazidi kuja kupiga magoti utusaidie kupunguza au kuondoa kabisa kodi kwenye maeneo ambapo tunapata marupurupu nje ya mshahara kama nauli za likizo, na overtime (muda nje ya kazi),” amesema. 

Kauli mbiu ya Mei Mosi ya mwaka huu wa 2023 ni  “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa.”

Wafanyakazi kutoka Wizara, Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi wakiwa kwenye Maandamano wakati wakiingia kwenye uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa yamefanyika Mkoani Morogoro tarehe 01 Mei, 2023. Picha | Ikulu.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV