Tucta uso kwa uso na taasisi za Serikali kuboresha maslahi ya wafanyakazi

May 5, 2023 11:27 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na maagizo ya Rais Samia katika maadhimisho ya Mei mosi
  • Masuala ya mishahara pamoja na kodi kujadiliwa.
  • Wafanyakazi watakiwa kuongeza tija ili madai ya nyongeza ya  mishahara yawe na hoja.

Dar es Salaam. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema lipo mbioni kuanza mchakato wa kufanya majadiliano na taasisi mbalimbali za Serikali kushughulikia  changamoto zinazowakabili wafanyakazi nchini ili kuboresha maslahi yao.

Hatua hiyo inakuja ikiwa zimepita siku nne tu tangu  Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atoe agizo hilo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Mei Mosi yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Said Wamba, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Tucta aliyekuwa akizungumza na wanahabari katika ofisi za shirikisho hilo leo Mei 5, 2023 amebainisha kuwa miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na masuala ya mishahara ya wafanyakazi kwa sekta binafsi na umma pamoja na kodi.

“Moja ya matatizo makubwa sana ya wafanyakazi nchi hii ni pamoja na kodi, kodi ni kubwa, na hawawezi kukwepa kulipa kwa sababu kipato chao kinajulikana na tegemeo kubwa sana na Serikali ni kupata kodi kutoka kwa wafanyakazi,” amesema Wamba jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi:


Wamba ameongeza kuwa tayari wameshapeleka mapendekezo Serikalini ya kupitia upya kodi zinazotozwa kwenye mishahara ili kumpunguzia mzigo mfanyakazi kwani hata kama mishahara itaongezwa bado tija yake haitaonekana kama itakatwa kiwango kikubwa cha kodi.

Wafanyakazi wakumbushwa kuongeza tija

Pamoja na kuwa wafanyakazi hususani wa sekta binafsi kuwa na malalamiko ya kutolipwa stahiki zao kwa wakati au kuendana na kazi wanayofanya, Wamba ametoa wito kwa wafanyakazi kuongeza tija kwenye utekelezaji wa majukumu yao ili madai yao yawe na mashiko.

“Nitoe wito kwa wafanyakazi nchini, waongeze tija ili tuwe na nguvu ya kudai mishahara, haitoshi kudai mishahara, lazima mishahara tunayodai itokane na tija ambayo tutakuwa tumeiwekeza sehemu zetu za kazi,” amesisitiza Wamba.

Itakumbukwa Disemba 2022,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi ambacho kimeanza kutumika rasmi Januari Mosi 2023.

Licha ya kima hicho ambacho hakikutangazwa tangu mwaka 2013 kupokelewa vema na baadhi ya watu, Tucta wamesema hatua hiyo ilikiuka taratibu kwani kiwango hicho kilipaswa kutangazwa kabla ya kuanza kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW