Mei Mosi 2023: Macho na masikio kwa Rais Samia

May 1, 2023 4:30 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na tamko la Serikali kuhusu nyongeza ya mishahara na kupunguza kodi ya mshahara.
  • Kima cha chini kwa watumishi wa umma ni jambo linaloweza kujitokeza.
  • Sherehe za Mei Mosi za mwaka huu zitafanyika Morogoro. 

Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki saa chache kabla ya kufanyika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yapo mambao kadhaa yakajitokeza katika sherehe za mwaka huu. 

Katika sherehe hizo zitakazofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro zimeandaliwa na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.  

Hiyo itakuwa mara ya tatu kwa Rais Samia kuhudhuria sherehe hizo tangu aapishwe kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka 2021 akichukua nafasi ya Hayati John Magufuli. 

Kauli mbiu ya Mei Mosi ya mwaka huu wa 2023 ni  “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa.”

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwasa amesema kuwa mkoa huo umejipanga vizuri katika kufanikisha sherehe hiyo muhimu kwa kuzingatia mambo matano ya msingi ikiwemo kuratibu suala la rasilimali fedha za maandalizi na kuandaa uwanja wenye hadhi.

Pia kuhamasisha wananchi kushiriki kwa shamrashamra kuelekea siku hiyo na kutangaza maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) pamoja na wajumbe wa kamati wakiwa katika ukaguzi wa maandalizi ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa. Wa pili kutoka kulia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Wakati wafanyakazi wakisubiri kwa shauku Serikali itasema nini kuhusu maslahi na mustakabali wa ajira zao, www.nukta.co.tz tunakuletea mambo kadhaa ambayo yanaweza kuteka ajenda za maadhimisho hayo na ambayo wafanyakazi wanayasubiri kuyasikia.

Kodi ya mishahara ya wafanyakazi

Katika sherehe za Mei Mosi mwaka 2021, Rais Samia alitangaza kupunguza kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) kutoka asilimia 9 ya wakati huo hadi asilimia 8 kilichoanza mwaka wa fedha wa 2021/22.

Hata hivyo, kwa mujibu wa viwango vya kodi vilivyopo sasa, punguzo hilo linawabeba zaidi wafanyakazi wa kada ya chini wanaolipwa mshahara unaozidi Sh270,000 hadi Sh520,000.

Lakini kwa wafanyakazi wanaolipwa mshahara zaidi ya Sh520,000 na kuendelea wanalazimika kulipa kodi ya ziada ukiondoa kodi ya msingi ya asilimia nane.

Kodi katika mishahara ya asilimia nane inayotumika sasa itapungua au itaongezeka? Tusubiri Mei Mosi. 


Soma zaidi: 


Nyongeza na kima cha chini cha mishahara kitakuwepo?

Mwaka jana, Serikali ya Tanzania ilitangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa umma kwa asilimia 23.3.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza Julai 29, 2022 jijini Dodoma alisema kuwa nyongeza ya mishahara iliwalenga zaidi wafanyakazi wanaopokea kima cha chini cha mshahara na siyo wafanyakazi wote.  

“Ni kweli asilimia 23 iliyotamkwa haijalipa watu wote, na hii ni kwa sababu ya formula inayotumika katika kutamka viwango vya Mshahara. Inapotamkwa wanaonufaika si wote mpaka wa mishahara mikubwa, bali ni wale wa kada ya chini,” alisema Majaliwa.

Amesema wanaonufaika ni wale wa kada ya chini, ambao kwa tangazo la mwaka huu wanufaika ni asilimia 75 hadi 78 ya watumishi wote.

Amesema nyongeza hiyo itawafaidisha zaidi wafanyakazi wa kada ya chini ili wawezesha kuboresha maisha yao katika kipindi hiki ambacho karibu kila bidhaa imepanda bei, jambo linaloongeza ukali wa maisha.

Mwaka huu Serikali itawakumbuka wafanyakazi na kuwaongezea kima cha chini na nyongeza ya mshahara?

Madaraja ya wafanyakazi wa umma

Septemba 2022, Serikali iliwapandisha madaraja watumishi 262,800 ambao kwa miaka mitano walikuwa hawajapanda huku ikitumia Sh58.3 bilioni kulipa mishahara kwa watu waliopandishwa. 

Pia aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama Oktoba 19, 2022 alisema katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 watumishi 120,210 wametengewa fedha ili wapandishwe madaraja. 

Suala la  upandishwaji madaraja/vyeo kwa watumishi wa umma linazingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utendaji kazi mzuri, kukidhi sifa zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, uwepo wa nafasi wazi na bajeti iliyotegwa. 

Sherehe za Mei Mosi za mwaka huu kutakuwa na matumaini yoyote kwa wafanyakazi kupanda madaraja?

Enable Notifications OK No thanks