Tanzania yaongeza mishahara kwa watumishi wa umma
- Uamuzi huo mpya wa Serikali utaongeza matumizi ya Serikali kwenye mishahara kwa Sh1.59 trilioni.
- Sasa kima cha chini kinatarajiwa kuwa zaidi ya Sh380,000 kwa mwezi kutoka Sh310,000 cha sasa.
- Watumishi wa umma walikuwa hawajapandishiwa mishahara kwa zaidi ya miaka mitano.
Dar es Salaam. Watumishi wa umma ni miongoni mwa watu watakaolala kwa furaha Tanzania baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia kupandishwa kwa mishahara na kima cha chini kwa asilimia 23.3, uamuzi utakaongeza matumizi ya Serikali kwenye mishahara kwa Sh1.59 trilioni.
Uamuzi huo, kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, umefanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP), matarajio ya mapato ya ndani ya mwaka 2022/23 na hali ya uchumi wa ndani na wa nje ya nchi.
Ongezeko hilo la kima cha chini la asilimia 23.3 litaongeza kiwango hicho kufikia Sh382,230 kwa mwezi kutoka Sh310,000 kinachotumika kwa sasa. Hii ina maana kima cha chini kitaongezeka kwa zaidi ya Sh70,000 kutoka kiwango kinachotumika mwaka huu wa fedha.
“Kutokana na hatua hiyo katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh9.7 trilioni kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za mitaa, taasisi na wakala wa Serikali,” imeeleza taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Zuhura Yunus, uamuzi huo utafanya bajeti ya mishahara kwa watumishi wa umma iongezeke kwa Sh1.59 trilioni mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 19.5 kutoka bajeti ya sasa inayoishia Juni 30.

Rais Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo wakati akizungumza na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Museveni katika Ikulu ya Entebbe Mei 10, 2022. Picha|Ikulu.
Watumishi wa umma kwa muda mrefu wamekuwa wakiilalamikia Serikali kwa kutoongeza mishahara yao kwa zaidi ya miaka mitano sasa licha ya gharama za maisha kuendelea kupanda kila uchao.
Yunus amesema mapendekezo hayo yaliyowasilishwa Ikulu jijini Dar es Salaam ni mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alichofanya hivi karibuni mkoani Dodoma na kupokea taarifa ya wataalamu kuhusu nyongeza ya mishahara.
Sanjari na nyongeza ya mishahara, Rais Samia ameridhia mapendekezo ya kanuni mpya za mafao ya pensheni na kuielekeza wizara inayosimamia hifadhi ya jamii na wadau wake kukamilisha taratibu za kuongeza malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 hadi asilimia 33.
Malipo ya mkupuo ya asilimia 25 ni moja ya masuala yaliyopingwa vikali wakati serikali inaboresha Sheria za hifadhi za jamii mwaka 2018 kiasi cha kulifanya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kuomba tena ongezeko Mei mosi mwaka huu.
Maboresho hayo ya utaratibu wa kulipa kwa mkupuo, yatafanya wastaafu kuweka kibindoni theluthi moja ya pensheni yao tofauti na sasa ambapo wanapata robo ya walichojihifadhia.
Uamuzi huo wa Serikali umepokelewa vema baada ya watu kuisifu Serikali huku wengine wakieleza kuwa hakuna sababu ya kuisifu kwa kuwa wafanyakazi hawakupandishiwa mishahara kwa muda mrefu.
Latest