Nyongeza ya mshahara: Rais Samia kutimiza ahadi yake Mei Mosi?
- Wafanyakazi wasubiri kwa hamu kauli yake juu ya mishahara.
- Wengine wataka kuboreshewa mazingira ya kazi.
- Kupanda kwa bei ya bidhaa kwa waweka katika wakati mgumu.
Mwanza/Dar es Salaam. Macho na masikio ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi yataelekezwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi sherehe za Mei Mosi mwaka huu huku baadhi ya wafanyakazi wakiwa na matumaini makubwa ya kupata nyongeza ya mishahara.
Hiyo itakuwa mara ya pili kwa Rais Samia kuhudhuria sherehe hizo tangu aapishwe kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka 2021 akichukua nafasi ya Hayati John Magufuli.
Macho na masikio ya wafanyakazi yatakuwa kwake ili kufahamu atazungumza nini kuhusu maslahi na mustakabali wa ajira zao hasa kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta ya umma na ile ya sekta binafsi na kupandisha madaraja wafanyakazi wa umma.
Jambo lingine ambalo litaibua mjadala katika sherehe hizo ambazo zinazofanyika kila mwaka ni nyongeza ya mishara kwa watumishi wa umma na kupungua kwa kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) ambacho kwa sasa ni asilimia nane kilichoanza kutumika mwaka jana.
Swali linabaki, Rais atatimiza ahadi yake aliyoitoa mwaka jana katika sherehe za Mei Mosi za mwaka jana zilizofanyika kitaifa mkoani Mwanza?
Rais Samia alisema hawezi kuongeza mishahara ya wafanyakazi hadi mwaka huu wa 2022 kutokana na kuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo za uchumi na janga la Corona (Uviko-19).
Pia alisema alishindwa kuongeza mishahara kutokana na hatua anazopanga kuchukua za kufuta kodi na tozo zilizokuwa zinawabughudhi Watanzania zilizosababisha kupungua kwa mapato yatokanayo na kodi.
“Lakini niwahakikishie wafanyakazi wenzangu kuwa mwakani siku kama ya leo (Mei Mosi 2022) nitakuja na package (kifurushi) nzuri ya kupandisha mishahara,” amesema Rais Samia katika hutuba yake ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na watu wengi hasa wafanyakazi.
Baadhi ya wafanyakazi walioshiriki sherehe za Mei Mosi mwaka jana mkoani Mwanza. Picha| Ikulu.
Kwa miaka zaidi ya sita sasa watumishi wa umma na sekta binafsi wamekuwa wakilalamikia kutopandishiwa mishahara na kuwa na maslahi duni licha ya gharama za maisha kupanda kila siku.
Huenda wakafutwa machozi katika sherehe za mwaka huu, kama walivyo na matarajio makubwa ya kuboresha maisha yao.
Baadhi ya wafanyakazi walioongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz), wamesema hali ya maisha imekuwa ngumu kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa kuliko sababishwa na athari za Uviko-19 na vita kati ya Ukraine na Urusi, huku wakibainisha kuwa nyongeza ya mishahara inaweza kuwafuta machozi.
“Hali ni ngumu, Serikali itoe ahueni, hatujapandishiwa mishahara kwa muda mrefu na sisi ni watu tunaostahili haki za msingi,” amesema mmoja wa walimu katika Shule ya Msingi ya Mkoani ya jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Matarajio mengine ambayo wafanyakazi wanatamani kuona waajiri katika sekta binafsi wakitoa ushirikiano kwa wafanyakazi wao katika nyanja zote lakini kuwaruhusu kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
Mmoja wa wafanyakazi katika kiwanda cha Nyakato Steel jijini Mwanza, Anord Kwilekwa amesema bado kuna wafanyakazi hawana mikataba ya moja kwa moja ambao wanalipwa kwa siku na wenye mikataba inayoanzia miezi mitatu na kuendelea ambao nao hawalipwi kiwango kikubwa cha fedha.
Soma zaidi:
- Wafanyakazi wengi hawajui haki zao: Ripoti
- Maswali manne yanayosubiri majibu sherehe za Mei Mosi 2019
- Kodi ya mshahara yapunguzwa Tanzania, nyongeza ya mshahara mwakani
Vyama vya wafanyakazi vyatoa neno
Vyama vya wafanyakazi Mkoani Mwanza vimesema katika maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu wanatarajia kuona Rais akitoa neno la matumaini kuhusu nyongeza ya mishahara.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Mwanza (TUCTA), Yusuph Simbauranga amesema kiu ya wafanyakazi katika maadhimisho ya mwaka huu ni kuona mishahara inapandishwa ili waweze kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.
“Ni zaidi ya miaka nane sasa hatujashuhudia serikali au sekta za umma zikipandisha mishahara, licha ya hali ya maisha kupanda, kima cha chini cha mshahara kimeendelea kubaki hicho hicho cha Sh80,000 hadi 100,000,” amesema Simbauranga.
Amesema matarajio kwa mfanyakazi wa kawaida kwa sekta binafsi kima cha chini kianzie Sh450,000 na kuendelea ambacho kitasaidia kupunguza ukali wa maisha.
Amesema mwaka huu wafanyakazi wana matarajio makubwa kwa kuwa katika maadhimisho ya mwaka jana katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza, Rais Samia Suluhu Hassan aliomba apewe muda ili aangalie namna ya kushughulikia suala hilo.
“Kwa maana hiyo wafanyakazi wana imani kubwa ya mishahara yao kupanda na kama ikitokea tofauti wataumia sana, kwa kuwa wafanyakazi tunapitia hali ngumu ya maisha, gharama za bei ya bidhaa zimekuwa juu,” amesema Simbauranga.
Katika maadhimisho hayo pia wanatarajia kuona Rais akizuia upandaji wa bidhaa usiozingatia utaratibu.
“Hivi sasa bei za bidhaa zimekuwa juu tunamuomba Rais pamoja na kupandisha mshahara lakini pia aangalie namna ya kuzuia kupanda kwa bei za bidhaa sokoni,” amesema.
Kauli mbiu ya sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi ) Mwaka huu ni “Maslahi bora, mishahara juu, kazi iendelee”
Habari hii imeandikwa na Daniel Samson na Mariam John.