Kodi ya mshahara yapunguzwa Tanzania, nyongeza ya mshahara mwakani

May 1, 2021 12:56 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan alipohudhuria sherehe za Mei Mosi jijini Mwanza leo. Picha|Ikulu.


  • Kodi hiyo inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi imepungua kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane.
  • Athari za Corona katika uchumi zazuia nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi. 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan leo ametangaza kuwa Serikali imepunguza kodi ya mshahara hadi kufikia asilimia nane huku akiahidi kupandisha mishahara ya wafanyakazi mwakani baada ya ugonjwa wa corona kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania. 

Katika hotuba yake ya katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mkoani Mwanza leo (Mei Mosi, 2021) Rais Samia amesema kodi ya mshahara (PAYE) inayotozwa kwenye mishahara ya wafanyakazi wa umma na binafsi imepunguzwa kutoka asilimia tisa ya awali hadi asilimia nane.

Punguzo hilo lililotangwaza leo katika hotuba hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wafanyakazi ni sawa na asilimia moja ya kodi. 

Mara ya mwisho Serikali ilipunguza kiwango cha PAYE katika mwaka wa fedha wa 2016/17 kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa na tangu hapo, miaka mitano sasa, haijawahi kubadilika. 

“Serikali imesikia ombi la wafanyakazi la kutaka kupunguziwa kodi inayotozwa kwenye mshahara (PAYE) na pia kutokukatwa kodi kwenye stahiki nyingine zisizokuwa za mshahara,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa na wahudhuriaji waliokuwepo katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 

Kwa mujibu wa viwango vya kodi vilivyopo sasa, punguzo hilo la kodi litawabeba zaidi wafanyakazi wa kada ya chini wanaolipwa mshahara unaozidi Sh270,000 na usiozidi Sh520,000. 

Lakini kwa wafanyakazi wanaolipwa mshahara zaidi Sh520,000 na kuendelea wanalazimika kulipa kodi ya ziada ukiondoa kodi ya msingi ya asilimia nane inayoongezeka kutokana na madara ya viwango vya mishahara. 

Mabadiliko hayo ya kodi yanatarajiwa kufanywa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22. 


Soma zaidi: 


Nyongeza ya mishahara mwakani

Kinyume na matarajio ya wafanyakazi wengi, Rais Samia amesema mwaka huu hawezi kuongeza mishahara ya wafanyakazi hadi mwakani kutokana na kuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo za uchumi na janga la Corona. 

“Nataka nitamke wazi mimi binafsi natamani kuona mishahara ya watumishi ingeongezwa ila kutokana na sababu mbalimbali nimeshindwa kutimiza matamanio yenu kwa mwaka huu.

“Kama mnavyofahamu kutokana na mlipuko wa Corona, kasi ya ukuaji wa uchumi duniani imeshuka. Kwetu Tanzania kasi ya ukuaji uchumi imepungua kutoka wastani wa asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7 mwaka huu,” amesema Mama Samia. 

Pia amesema ameshindwa kuongeza mishahara kutokana kutokana na hatua anazopanga kuchukua za kufuta kodi na tozo zinazobughudhi Watanzania zilizosababisha kupungua kwa mapato yatokanayo na kodi.

“Lakini niwahakikishie wafanyakazi wenzangu kuwa mwakani siku kama ya leo nitakuja na package nzuri ya kupandisha mishahara,” amesema Rais Samia katika hutuba yake ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na watu wengi hasa wafanyakazi.

Kwa miaka zaidi ya sita sasa watumishi wa umma na sekta binafsi wamekuwa wakilalamikia kutopandishiwa mishahara na kuwa na maslahi duni licha ya gharama za maisha kupanda kila siku. 

Kama hukupata fursa ya kufuatilia mubashara sherehe za Mei Mosi unaweza kutaza hapa

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN MGENI RASMI MAY MOSI, MWANZA https://t.co/1XsHzWhgVm

Wafanyakazi wanena

Wakizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz)  baada ya kukamilika kwa hotuba ya Rais Samia, baadhi ya wafanyakazi wameeleza kuwa pamoja na kutopandishwa mishahara lakini wanashukuru kwa kupunguziwa baadhi ya mambo ikiwemo suala la kodi ya mshahara na tozo ya kutunza thamani ya mkopo wa Bodi ya Mkopo ya Elimu ya Juu Tanzania (HESLB).

“Tunashukru licha ya kushindwa kupandisha mshahara lakini kuna mambo ameyaondoa na mengine kupunguza likiwemo hilo la kodi ya elimu ya juu ambayo imeshushwa kwa asilimia 6,” amesema Mashauri Mashalaa ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Misasi jijini Mwanza. 

Naye Mkurungezi wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea haki za wafanayakazi wa nyumbani la Wote sawa, Angela Benedictor amesema bado wana matumaini makubwa kuwa rais ataongeza mishahara mwakani kama alivyosema.

“Tumpe muda tuna imani atapandisha mishahara kwa wafanyakazi lengo ni kuhakikisha tunashiriki kwa pamoja kufikia uchumi wa juu,” amesema Benedictor.

Nyongeza na Mariam John kutoka Mwanza

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW