Kitendawili, hesabu ikiwatoa jasho watahiniwa kidato cha nne 2025
- Ufaulu waendelea kuwa chini ya wastani licha ya juhudi za Serikali
- Wadau wa elimu wapendekeza matumizi ya mbinu shirikishi kuongeza ufaulu.
Dar es Salaam. Huenda Serikali na wadau wa elimu nchini wakawa na kibarua cha kutafuta mwarobaini wa kuongeza ufaulu wa somo la Hesabu mara baada ya ufaulu wa somo hilo kusalia chini ya viwango kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Prof Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo Januari 31, 2026 amesema kuwa ufaulu wa somo hilo kwa mwaka 2025 ni asilimia 26.45.
“Kwa upande wa somo la basic mathematics (hesabu) ufaulu umeendelea kuwa chini ya wastani kwa mwaka 2025 kama ilivyokuwa mwaka 2024, 2023, 2022,” amesema Prof Mohamed.
Kwa mujibu wa Necta, Mwanafunzi atahesabiwa kufaulu somo endapo atapata angalau alama ya D ambao ni kuanzia alama 30 na kuendelea, hatua ambayo haijawahi kufikiwa katika somo la hesabu kwa zaidi ya miaka 10.
Takwimu hizo za ufaulu somo la hesabu ni sawa na kusema zaidi ya wanafunzi saba kati ya 10 waliofanya mtihani wa somo hilo mwaka 2025 walifeli hesabu kwa kupata daraja F suala linaloweza kuwanyima kujiunga na baadhi ya tahasusi na kozi zinazohitaji ufaulu wa somo hilo katika ngazi za elimu ya juu.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari katika matokeo ya miaka 10 iliyopita unaonesha kupanda na kushuka kwa ufaulu wa somo hilo licha ya kuendelea kuwa chini ya viwango.
Mathalani, mwaka 2015 ufaulu ulikuwa asilimia 16.76, na miaka iliyofuata uliongezeka kwa taratibu hadi asilimia mwaka 2019 ulipofikia asilimia 20.03.
Mwaka 2020 ufaulu huo uliongezeka tena kufikia asilimia 20.12 kabla ya kushuka mwaka 2021 mpaka asilimia asilimia 19.6 na kupanda tena kidogo mwaka 2022 hadi asilimia 21.1.
Kadhalika mwaka 2023 ufaulu ulipanda kwa asilimia nne na kufikia asilimia 25.42, lakini ulidorora tena mwaka 2024 hadi asilimia 25.35 kabla ya kuongezeka tena mwaka 2025.

Mbinu bora za ufundishaji wa somo la hesabu kuanzia ngazi ya awali zinaweza kusaidia kuongeza ufaulu wa somo hilo kwa miaka ijayo.PichaMwanga TV
Tumaini lachomoza wachambuzi wakieleza sababu
Licha ya ufaulu wa somo hilo kuendelea kuwa chini ya viwango, mwaka 2025 ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 1.1 suala linalotoa dalili chanya kuwa huenda hhuo ukawa mwanzo wa ufaulu wa somo hilo kuinuka.
Ili kufahamu ukweli wa mambo na sababu ya ufaulu wa somo hilo kuendelea kudorora, Nukta Habari imezungumza na Mwalimu Veronica Sarungi kutoka Shule ya Sekondari Aga Khan Mzizima akieleza kuwa huenda mada zisizo za lazima katika somo hilo zikawa sababu ya ufauluu kushuka.
“Hesabu ni somo linalohitaji mwalimu awe karibu sana na mwanafunzi, na ukosefu wa walimu unazidi kufanya somo hili kuwa gumu zaidi,” aliongeza Sarungi.
Hata hivyo, Sarungi ambaye amewahi kuwa mwanafunzi bora wa kidato cha nne mwaka 1989 ametoa wito kwa walimu kuongeza juhudi za kuondoa daraja la F kwa wanafunzi wote, badala ya kuwekeza juhudi kwa kundi dogo linaloweza kupata daraja A kwa ajili ya zawadi.
“Tunapaswa kutumia vipindi vya mtandaoni na mbinu za kisasa za kufundishia ili kuwafanya wanafunzi wapende hesabu. Pia, wazazi na walimu wanapaswa kushirikiana badala ya kurushiana lawama,” amesisitiza Sarungi.
Latest